SERIKALI imesema kuna ongezeko la viumbe vamizi hasa magugu maji katika vyanzo vya maji nchini, hali inayotishia kuongezeka kwa uhaba wa mazalia ya samaki na hatari ya viumbe wanaoishi katika magugu, kuwadhuru raia wanaokaa maeneo ya karibu na vyanzo hivyo.
Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis, aliyasema hao jana bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Costantine Kanyasu.
Katika swali hilo, Kanyasu alitaka kujua ni kwa namna gani serikali inafahamu ongezeko la magugu maji Ziwa Victoria na zipi athari zake na mpango wa kuyadhibiti.
Khamis alisema serikali inafahamu ongezeko la magugu maji katika Ziwa Victoria ambayo yamesababisha athari za kimazingira, kiuchumi na kijamii ikiwamo kupungua kwa oksijeni ambayo huzuia mzunguko wa hewa na mwanga wa jua hatimaye kusababisha vifo vya samaki.
Alisema mkakati na mpango kazi wa kukabiliana na viumbe vamizi wa mwaka 2019-2029, unatoa mwongozo namna ya kuzuia kuingia na kuenea kwa viumbe vamizi na una mpango wa kushughulikia viumbe vamizi walioko na wanaoweza kuingia.
Khamis alisema wanatoa elimu na kuwajengea uwezo wananchi wanaoishi karibu na ziwa kwa namna ya kujitolea katika kazi za kutokomeza na kuenea kwa magugu maji kila yanapojitokeza..
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge Kanyasu, alililouliza kuhusu njia mbadala ya haraka katika kuokoa Ziwa Victoria, alisema uwapo magugu maji si jambo la kufanya leo kwa sababu limeenea katika vyanzo vingi vya maji, hivyo alimwomba mbunge huyo kuwa mvumilivu wakati serikali ikiendelea na tathmini.
Kuhusu mpango wa serikali wa kuondoa tope lililojaa katika Bwawa la Kalemawe, wilayani Same, alisema serikali inakamilisha usanifu wa kina na kuandaa gharama za kulikarabati.
Alisema kupitia Wizara ya Maji, serikali imetenga Sh. bilioni moja, zitakazotumika kujenga msingi wa tuta la bwawa hilo, kazi ambayo imepangwa kuanza kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED