Mradi Bwawa la Nyerere kukamilika Februari

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 08:53 AM Feb 01 2025
Mradi Bwawa la Nyerere.
Picha: Mtandao
Mradi Bwawa la Nyerere.

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere utakamilika rasmi mwishoni mwa Februari, mwaka huu, baada ya kukabidhiwa mtambo wa tisa wa kuzalisha umeme.

Akichangia jana bungeni azimio la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa nishati Afrika, Dk. Biteko alisema bwawa hilo lilipaswa kukamilika ifikapo Mei mwaka huu.

“Hadi leo asubuhi mitambo yote minane imekabidhiwa na mtambo mmoja, ambao ni  wa tisa, utakabidhiwa mwishoni mwa Februari, mwaka huu, na mradi wa bwawa hili tutakuwa tumemaliza,” alisema.

Dk. Biteko pia alisema mpango wa nishati umetoa viashiria vitano kikiwamo cha upatikanaji wa umeme kwa Tanzania kwa asilimia 78.4.

Alisema katika mpango huo walitia saini miaka mitano ijayo Tanzania itafikia upatikanaji wa umeme kwa asilimia 100.

“Uunganishaji umeme na wateja leo tunapozungumza hatua tuliyo nayo, tumeunganisha wateja milioni 5.5 na mpango ni kupeleka kwa wateja milioni 13.5 na usingekuwa mpango huo wangepambana na wasingezidi milioni 5.2,” alisema.

Alisema kuwa kwenye nishati safi ya kupikia wanataka watoke asilimia 9.9 kwenda asilimia 75 ndani ya miaka mitano.

“Mchango wa nishati jadidifu itoke asilimia 56 iliyopo twende asilimia 65 na tutalifikia suala hili bila wasiwasi wowote,” alisema.

Biteko alisema mkutano huo ulikuwa na mwitikio mkubwa wa watu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia.

“Sababu mbili zilizofanya mkutano huu kuja Tanzania ni kuimarika kwa diplomasia yetu na mataifa mengine na haijaimarishwa na mwingine ni yeye Rais Samia. Kasi  kubwa ya upelekaji umeme kwa wananchi hasa vijijini, Benki ya Dunia walivyofanya tathmini mwaka jana Tanzania iliongoza na wakaona mahali pekee pakupeleka mpango huu ni Tanzania,” alisema.

Alibainisha kuwa Rais Samia ametoa msukumo mkubwa kwenye sekta ya nishati na kuahidi makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano huo atayasimamia na hayatabaki kwenye makaratasi.

Naye Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson,  alipongeza serikali kwa kukamilisha mradi wa Nyerere kabla ya muda uliopangwa na kwamba fedha zilizokuwa zinaelekezwa kwenye masuala ya umeme sasa zitapelekwa miradi mingine ikiwamo barabara ambazo wabunge wamekuwa wakipigia kelele.