Mpango kituo forodha Kabanga kufanya kazi saa 24

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:47 AM Feb 01 2025
Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande.
Picha: Bungeni
Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande.

SERIKALI imesema inafanya jitihada ili Kituo cha Forodha cha Pamoja (OSBP) Kabanga, kinachotoa huduma kati ya Tanzania na Burundi, kufanya kazi kwa saa 24 ili kuongeza ufanisi.

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, alisema hayo juzi alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ngara, Ndaisaba Ruhoho, aliyetaka kujua mkakati wa serikali wa kuwezesha vituo vya forodha vya Murusagamba na Kabanga, kufanya kazi kwa saa 24.

 Chande alisema kuwa Kituo cha Forodha cha Kabanga ni Kituo cha Pamoja (OSBP) cha kutoa huduma za forodha kati ya Tanzania na Burundi kina miundombinu wezeshi kama vile taa za ulinzi, vyombo vya ulinzi na usalama, na maeneo ya kukagulia bidhaa, wasafiri na wafanyakazi, hivyo kuwa na uwezo wa kufanya kazi saa 24 kwa upande wa Tanzania.

“Ili kituo hicho kitoe huduma saa 24, upande wa Kobero nchini Burundi unapaswa pia kuwa tayari kutoa huduma hizo saa 24”, alisema. 

Chande alisema kwa sasa Kituo cha OSBP Kobero kwa upande wa Burundi kinatoa huduma kwa saa 12 tu, hivyo jitihada mbalimbali zinaendelea kufanyika ili kuwezesha mazingira ya kituo hicho kufanya kazi saa 24, hususan ulinzi na usalama.

Kuhusu kituo cha Murusagamba, Chande alisema hicho ni kidogo cha forodha kinachofanya kazi ya uzuiaji na hufanya kazi ya kuzuia magendo kwenye maeneo ambayo mwenendo wa bidhaa na watu ni mdogo.

Naibu Waziri Chande alisema kutokana na udogo wa mwenendo wa bidhaa na watu katika kituo cha Murusagamba, uwezekano wa kituo hiki kufanya kazi saa 24 kwa sasa haupo.

Akijibu maswali ya nyongeza kuhusu ufungaji wa kifaa cha ukaguzi eneo la Mutukula lililoko mpaka wa Tanzania na Uganda na Kituo cha Horohoro, Tanga kati ya Tanzania na Kenya, Chande alisema kwa upande wa Mutukula tayari mkandarasi yuko eneo la mradi kwa ajili ya kufunga kifaa hicho na upande wa Horohoro, serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaangalia utekelezaji wake.

Pia alisema mazungumzo yanaendelea kuhusu uwezekano wa Kituo cha Forodha cha Malindi, Zanzibar kufanya kazi saa 24 kwa kuwa kwa sasa kinahudumia makontena 2,000 kwa mwezi licha ya kufanya kazi kwa saa 12.

Alisema serikali inaendelea na mazungumzo na upande wa Zanzibar na kwamba kukamilika kwa mazungumzo hayo kutawezesha huduma hiyo.