Wakuu wa SADC walaani mapigano DRC

By Restuta James , Nipashe
Published at 08:42 AM Feb 01 2025
Wakuu wa SADC walaani mapigano DRC
Picha:Mtandao
Wakuu wa SADC walaani mapigano DRC

WAKUU wa nchi na serikali kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), wamelaani vita vinavyoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) huku wakisisitiza dhamira yao ya kuhakikisha usalama na amani ya kikanda.

Viongozi hao waliitisha mkutano wa dharura jana Harare, Zimbabwe, kwa lengo la kujadili hali ya usalama katika eneo hilo.

Mkutano huo uliongozwa na Rais wa Zimbabwe na Mwenyekiti wa SADC, Dk. Emmerson Mnangagwa, ambaye katika hotuba yake ya ufunguzi, alisisitiza haja ya dharura ya kuimarishwa kwa juhudi za kujenga amani na mazungumzo ili kutatua mgogoro huo.

Alisema jukumu la SADC ni kujitolea kulinda amani na usalama wa kikanda na kuahidi kuongeza juhudi za kulinda raia kutokana na kukosekana kwa utulivu kwa mujibu wa Mkataba wa Ulinzi wa Pamoja wa SADC.

Rais Mnangagwa alisisitiza umuhimu wa kuimarisha utashi wa kisiasa katika eneo lote, kwa lengo la kutengeneza mkakati unaotekelezeka wa kuleta amani Mashariki mwa DRC.

Alishukuru juhudi za washirika wa kimataifa kuhusu mzozo huo na kusisitiza kuwa kazi kubwa zaidi inahitajika kufanywa ili kupunguza mateso ya watu waliokimbia makazi katika eneo hilo.

“Mzozo unaoendelea Mashariki mwa DRC, unaotokana na migogoro ya silaha inayoendelea, hauwezi kupuuzwa. Watu wa eneo hili wameteseka kwa muda mrefu sana,” Mnangagwa alisema.

Mkutano huo uliwakutanisha wakuu wa nchi kutoka nchi kadhaa wanachama wa SADC. Viongozi hao walionesha mshikamano usioyumba na watu wa mashariki mwa DRC na kusisitiza kujitolea kwao kutafuta suluhu za kudumu kwa ghasia zinazoendelea.

Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) alikuwa miongoni mwa wakuu wa nchi wanaoshiriki kikao hicho muhimu.

Aidha, Rais Felix Tshisekedi alihudhuria mkutano huo kwa mtandao.

Lengo kuu la mkutano huo wa dharura lilikuwa kuandaa mkakati wa kina wa amani, kutumia ushirikiano wa kikanda na msaada wa kimataifa, ili kurejesha amani ya kudumu na utulivu katika eneo lenye matatizo.

Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi, alisema kutokana na uzito wa hali ya usalama Mashariki mwa DRC, mkutano huo umeitishwa ili kutathmini na kuimarisha mwitikio wa pamoja wa amani na usalama nchini humo.

“Majadiliano katika mkutano huu yanathibitisha dhamira isiyoyumba ya SADC ya kusaidia DRC na kuhakikisha utulivu wa muda mrefu katika kanda.

“Nina imani kwamba uamuzi uliyofanywa hapa utaakisi mshikamano wetu unaoendelea na watu wa DRC na dhamira yetu pana ya kuimarisha usalama na utulivu katika eneo lote na bara.

 â€śUkanda wetu umejulikana kwa muda mrefu kwa kuishi kwa amani na ustahimilivu. Imesalia kuwa ni mwanga wa matumaini kwa watu wa SADC na Afrika kwa ujumla, hasa katika ulimwengu ambao wengi wanaendelea kustahimili athari mbaya za migogoro na ukosefu wa utulivu,” alisema.

Alisisitiza dhamira ya SADC ya amani ya kikanda, umoja na maendeleo, kuhakikisha kwamba, watu wa DRC na kanda nzima wanaweza kutazamia mustakabali wa amani, usalama na ustawi.

Mkutano huo unafanyika baada ya Mkutano wa Dharura wa Utatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi Usalama (SADC Organ Troika) na zinazochangia askari katika mpango wa SADC nchini DRC (SAMIDRC),  uliofanyika Januari 28, mwaka huu na kuongozwa Rais Samia.