KWA miaka ya hivi karibuni sasa kumekuwa kama kuna utamaduni hivi wa baadhi ya timu kuhitaji sare tu zikicheza dhidi ya Simba, Yanga au Azam FC.
Klabu zinazoitwa au kujiita ndogo, zimekuwa na mkakati wa kwenda kucheza na timu hizo si kupata ushindi, ila kuhitaji sare, na ukitaka kuona hilo, angalia hata dakika 20 tu za mwanzo utaona jinsi wachezaji wanavyopambana kuanza kupoteza muda.
Hawana haraka, wala hawahitaji kushinda, watafanya kila njia kupoteza muda kwa staili yoyote ile.
Kuanzia makipa mpaka wachezaji wa ndani hawatokuwa tena na hamu ya mpira, ila kuhakikisha dakika zinakwenda. Hali inabadilika tu pale ambapo timu kubwa zitakapopata bao. Hapo sasa ucheleweshwaji muda unakuwa umekufa labda baadaye wakisawazisha.
Binafsi, sijajua tabia ama staili hii imetokea wapi na imeanza vipi, kwani imekuwa haina afya na wakati mwingine kusababisha soka lisichezwe kwa muda unaotakiwa.
Mashabiki wanakuwa wametoka maeneo mbalimbali, wamelipa viingilio, wamelipia ving'amuzi kwa ajili ya kuutazama kwenye televisheni, lakini wanakutana na timu ambayo moja inataka kucheza soka, nyingine haitaki, ila imekuja pale kutimiza wajibu.
Ukitaka kuona ni kweli timu hizo zinahitaji sare, zikiipata zinavyoshangilia, kama kuna mgeni hajui chochote anaweza kudhani hiyo timu imeshinda mechi hiyo. Na itakavyozungumzwa ni kama imeshinda, huku timu kubwa ikionekana kama imefungwa.
Kwangu mimi naona hii ni hali ya kutojiamini, na tunawapa nguvu wale wanaosema kuwa ligi yetu ina ushindani dhaifu.
Kama timu inaingia uwanjani kwa lengo la kutafuta sare dhidi ya timu nyingine tena kwenye michezo ya Ligi Kuu ambayo si mtoano, bali zinatafutwa pointi tatu kama si udhaifu wenyewe ni nini?
Huwezi kuona kwenye ligi za wenzetu timu hata inayoshika mkia, inaingia uwanjani kucheza na inayoongoza ligi, au timu maarufu ikipoteza muda. Sana sana itakachofanya ni kucheza kwa nidhamu, kukaa nyuma ya mpira, lakini si kufanya kama tunavyoona kwenye Ligi ya Tanzania.
Halafu wakitokea waamuzi ambao hawakubaliani na hilo, wanapoongeza dakika nyingi na wakafungwa bao wanalalamika kuwa wameonewa.
Mimi nadhani pia hata hizi timu zinazopoteza muda zinajinyima zenyewe ushindi kwani kama zikiamua kushambulia na kutopoteza muda, zinaweza kupata ushindi dhidi ya timu kubwa.
Badala yake woga tu ndiyo unaowaponza. Utashangaa kuona hata baadhi ya timu za madaraja ya kati, ambazo zina wachezaji bora, nyota kutoka nje ya nchi wenye uwezo mkubwa, nao pia wanakuwa na muono ule ule tu wa kupoteza muda zinapocheza na Simba, Yanga au Azam.
Natambua kupoteza muda kupo, lakini ni kwenye michezo ya mtoano au mchezo huo timu inahitaji sare tu ili kusonga mbele, hapo kunakuwa na mantiki.
Mfano Waarabu wanaposaka sare ugenini ili kwenda kushinda kwao, huwezi kushangaa. Timu imeshinda ugenini mchezo wa kwanza na sasa inacheza nyumbani na sare inaweza kuivusha, hapo mantiki ipo, lakini ninachoshangaa mimi kwenye michezo ya ligi ambayo zinasakwa pointi tatu kwenye kila mchezo.
Nizishauri timu hizo hizo ziache tabia hiyo, kwani ninavyoona wakati mwingine zinakuwa na uwezo kabisa wa kuzifunga timu kubwa, ila woga ndiyo unaosababisha kutaka sare ambayo wakati mwingine haizipati.
Nikikumbuka miaka ya 1980, 1990, hadi 2000, kwenye michezo wa Ligi Kuu, huwezi kuona timu yoyote hata ndogo ikipoteza muda au kucheza kwa kutaka sare dhidi ya Simba au Yanga.
Zitacheza kama kawaida kama kufungwa itafungwa, kama kushinda itashinda na kama sare itatoka na wala hutaona wachezaji na viongozi wakishangilia sare.
Ndipo tuliposhuhudia kuwa haikuwa ajabu Pamba ikiifunga Yanga mabao 3-0, Reli ya Morogoro kuifunga Simba 5-2, Majimaji kuzifunga timu zote kubwa, Mecco kuzisumbua timu hizo kiasi cha wakubwa hao kuungana na kushtaki FAT, sasa TFF, kuwa wachezaji wa timu hiyo ya Mbeya wanatumia madawa ya kuongeza nguvu, wakidai huwa hawachoki, kumbe ni mazoezi tu.
Ni kipindi ambacho mashabiki wa Simba na Yanga, pamoja na kuwa na timu bora, lakini zilikuwa zikipata upinzani mkali kiasi kwamba kuna wakati timu imeshakula mabao 2-0, lakini wanaombea mpira uishe, hakuna kupoteza muda.
Tunahitaji tena timu za aina ile kama Sigara, Pilsner, Nyota Nyekundu, Ushirika ya Moshi, Tukuyu Stars, Milambo, RTC Kagera, Biashara Shinyanga, RTC Kigoma, ili watu washindane kambumbu uwanjani na si 'kautamaduni' haka kakupoteza muda.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED