Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amewapongeza wahitimu 110 wa mahafali ya 10 ya Programu ya Mwanamke Kiongozi na kuwasihi kuwa wabunifu na kuwa chachu ya maendeleo ya taifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rais Samia amewataka wahitimu hao kutumia ujuzi walioupata kwa kuwafungulia njia wengine, si wanawake pekee bali pia wanaume, kwa lengo la kujenga jamii yenye usawa na maendeleo jumuishi.
Aidha, amewahimiza kupuuza dhana potofu kwamba mwanamke ni mtu wa nyumbani pekee na hawezi kuwa kiongozi, akisisitiza kuwa wanawake wana uwezo sawa na wanaume katika nafasi mbalimbali za uongozi.
"Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu, hivyo niwaombe wanawake mjitokeze kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi sawa na wanaume. Pia, hakikisheni mnaandikishwa katika daftari la wapiga kura ili muwe na sifa ya kuchagua na kuchaguliwa," amesema Rais Samia.
Hafla hiyo imefanyika sambamba na Mkutano Mkuu wa Saba wa Mwaka, wenye lengo la kuwawezesha wanawake viongozi na wasichana, huku kaulimbiu ikiwa "Haki, Usawa na Uwezeshwaji."
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED