RAIS Samia Suluhu Hassan, juzi aliwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni ikiwa ni jitihada zake za kujaza ombwe la nafasi katika utendaji au mabadiliko ya kawaida kuimarisha utendaji ambayo amekuwa akiyafanya mara kwa mara.
Katika uapisho huo, waliohusika ni majaji wa Mahakama ya Rufani ambao walipandishwa kutoka kuwa majaji wa Mahakama Kuu. Mwingine aliyeapishwa ni Dk. Grace Magembe ambaye hivi karibuni aliteuliwa kushika nafasi hiyo kuchukua nafasi ya Prof. Tumaini Nagu ambaye uteuzi wake umetenguliwa. Kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo, Dk. Magembe alikuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Pamoja na kuwaagiza majaji kuwajibika na kuhakikisha haki inatendeka, kubwa zaidi aliloagiza ni kwa Dk. Magembe kwamba akasimamie udhibiti wa magonjwa ya mlipuko ambayo yana athari kubwa kwa nchi kiuchumi na kijamii.
Hivi karibuni, kwa mfano, kulikuwa na taarifa ya kuibuka kwa ugonjwa wa Malburg katika mkoa wa Kagera ambao ungesababisha watu kuzuiwa kusafiri hivyo kuwapo kwa athari kubwa. Ugonjwa huo uliwahi kuripotiwa mkoani humo na kusababisha vifo vya watu kadhaa.
Licha ya ugonjwa huo, mwaka 2020 uliibuka ugonjwa wa UVIKO – 19 ambao uliikumba dunia nzima na kusababisha vifo vya mamilioni ya watu, uchumi wa mataifa mbalimbali kuporomoka na watu kukosa kazi kutokana na uzalishaji kuwa mdogo na taasisi na mashirika makubwa kufungwa. Tanzania ilikuwa moja ya nchi zilizoathirika kwa kiasi kikubwa kwa kuwa watalii kutoka mataifa mbalimbali walishindwa kusafiri na kutembelea vivutio na mbuga za wanyama.
Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana Rais Samia amemwagiza Dk. Magembe kusimamia ipasavyo magonjwa ya mlipuko ili kuepukana na athari zinazoweza kujitokeza pindi magonjwa hayo yanapoibuka.
Licha ya magonjwa hayo makubwa ya mlipuko ikiwamo Ebola ambayo inaitesa nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), nchini Tanzania kila mwaka kumekuwa kukiripotiwa kuibuka kwa maradhi mengine ya mlipuko kama vile kipindupindu, kuhara na kuhara damu. Magonjwa hayo tariban kila mwaka yamekuwa yakiibuka maeneo mbalimbali ya nchi na sababu kubwa ni uchafu.
Ni dhahiri kwamba Rais Samia ameonesha kukerwa na kuwapo taarifa za mara kwa mara za magonjwa hayo, ndiyo maana ametoa agizo hilo kwa msisitizo mkubwa kwa sababu yana athari kubwa kwa uchumi wa nchi.
Ni kweli kwamba Rais Samia amemwagiza Dk. Magembe kusimamia suala hilo akiwa ndiye mganga mkuu kiongozi wa serikali lakini maana yake ni kwamba waganga wote wakuu wa mikoa na wilaya na wale wafawidhi wa hospitali na vituo vya afya wanahusika na jambo hilo.
Kwa maana hiyo, wote hao pamoja na viongozi waliopewa dhamana katika ngazi mbalimbali za serikali, wanatakiwa kuwajibika katika vita dhidi ya magonjwa hayo. Kushindwa kuwajibika kwao wanaweza kuchukuliwa hatua kali ikiwamo kuondolewa kwenye nafasi zao za kiutendaji.
Katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya kwa mfano, taarifa za magonjwa ya mlipuko ya kipindupindu, kuhara na kuhara damu yamekuwa yakiripotiwa takriban kila mwaka. Jambo la kujiuliza ni je, wahusika wameshindwa kusimamia ipasavyo suala la usafi mpaka maeneo hayo kuwa makao makuu ya kipindupindu?
Kuwapo kwa magonjwa hayo kila mwaka ni dhahiri kuna uzembe miongoni mwa watendaji kwa sababu wameshindwa kusimamia usafi wa mazingira na kuchukua hatua dhidi ya wananchi wanaotiririsha maji machafu nyakati za mvua. Kila mtu akiwajibika na kuwapo kwa dhamira ya dhati magonjwa hayo yatakuwa historia nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED