Samia ampa jukumu Mganga Mkuu kudhibiti magonjwa ya mlipuko

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 08:51 AM Jan 23 2025
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali baada ya kuwaapisha majaji wa Mahakama ya Rufani, Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma jana.
PICHA: IKULU
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali baada ya kuwaapisha majaji wa Mahakama ya Rufani, Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma jana.

RAIS Samia Suluhu Hassan amemtaka Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Magembe kudhibiti milipuko ya magonjwa inayoweza kusababisha nchi kuingia katika changamoto mbalimbali ikiwamo kuzuiwa kwa safari za kimataifa.

Alitoa agizo hilo jana Ikulu ya Chamwino, mkoani hapa, wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni.

Alisema nafasi ya Mganga Mkuu wa Serikali ni jukumu kubwa na anapaswa kwenda kushirikiana na timu yake kudhibiti milipo ya magonjwa nchini.

"Niwaombe viongozi mlioteuliwa na kuhamishwa vituo vyenu vya kazi hivi karibuni mnakwenda kutimiza majukumu yenu hususan nafazi ya Mganga Mkuu wa Serikali ni nafasi kubwa sana ambayo inahitaji umakini mkubwa sana.

"Sasa nikuagize Mganga Mkuu wa Serikali kuhakikisha unashirikiana na timu yako kwenda kuzuia milipuko ya magonjwa ambayo inayohofiwa kuifanya nchi yetu kutajwa na mataifa mengine kuwa ni sehemu ya milipuko ya magonjwa na kusababisha nchi yetu kufungiwa safari za nje," alisisitiza Rais Samia. 

Vilevile, aliwaagiza Majaji wa Mahakama ya Rufani aliowaapisha kwenda kuutumia vizuri uhuru wa muhimili huo kwa kutenda haki na sio vinginevyo.

"Uhuru wa muhimili wa mahakama uendelee kutumika vizuri kwa ajili ya kutoa haki kwa Watanzania wote na nyie mkawe sehemu ya mabadiliko katika maeneo yenu mliochaguliwa," alisema.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, alisema hatua ya Rais Samia kufanya uteuzi wa Majaji wa Mahakama ya Rufani kutasaidia kupunguza changamoto mbalimbali ikiwamo mlundikano wa mashauri pamoja na wafungwa na mahabusu.

"Mheshimiwa Rais uteuzi huu wa Majaji wa Mahakama ya Rufani umefanya idadi yao kuongezeka kutoka 35 hadi 39 hali hii inakwenda kusaidia kupunguza mrundikano wa mashauri pamoja na wafungwa na mahabusu.

"Mwezi Novemba, mwaka jana, nilitembelewa na Kamishna Jenerali wa Magereza akaniambia kuwa haya maboresho yanayofanywa na serikali ikiwamo ongezeko la majaji imewasaidia sana kupunguza sana mrundikano wa wafungwa na mahabusu," alisema.

Alisema, kwa mujibu wa Kamishna wa Magereza inao uwezo wa kuhifadhi wafungwa 29,000, lakini kutokana na uwekezaji katika muhimili wa Mahakama hivi sasa kuna nafasi ya wafungwa 2,000 ambayo ipo wazi.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Magembe, aliteuliwa hivi karibuni kushika nafasi ya Profesa Tumaini Nagu, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Samia.

Kabla ya kuteuliwa, Dk. Magembe alikuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.