MWENYEKITI wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) Deogratius Mahinyila amesema anatamani kuona Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Tundu Lissu anakiunganisha chama hicho ili kujiandaa na uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Akizungumza na Nipashe Digital katika ukumbi wa Mlimani City jana, Mahinyila alisema maelekezo yaliyotolewa na Mwenyekiti mstaafu, Freeman Mbowe kuhusu kutibu majeraha yaliyotokana na uchaguzi huo ni muhimu yakazingatiwa ili kuhakikisha wanachama wanarudi kuwa wamoja na kujiandaa na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
“Ninatamani kuona Mwenyekiti wetu mpya anakiunganisha chama na kumfanya kila mmoja ajisikie kuwa na amani katika hiki chama, bila kujali alikuwa anamuunga mkono nani , arudishe morali ya mapambano na umoja ndani ya chama” alisema Mahinyila.
Katibu wa BAVICHA Jimbo la Kibamba, Nice Sumari alisema anatamani kuona chama kinaendelea kudai haki ya vijana waliopotea katika mazingira tatanishi akiwemo Deusedith Soka ambaye amemaliza miezi kadhaa bila kuonekana ili kurejesha morali ya vijana kuendelea na mapambano ya kufanya siasa kwa amani.
“Chama hiki tumekijenga kwa maumivu makubwa na tutakilinda kwa wivu mkubwa ninatamani kuona tunaendelea kudai kupatikana kwa vijana wenzetu waliopotea akiwemo Deusdedith Soka na wenzake ambao mpaka sasa hatujui walipo” alisema Nice.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED