HISTORIA imeandikwa katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kupata mwenyekiti mpya baada ya miaka takribani 20 ya uongozi wa Freeman Mbowe.
Tundu Lissu anakuwa mwenyekiti wa nne katika historia ya CHADEMA baada ya kuwashinda Mbowe na Odero Charles katika uchaguzi uliofanywa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama usiku wa kuamkia jana na matokeo yake kutangazwa asubuhi ya jana.
Mchuano wa uchaguzi huo ulikuwa mkali, hasa kwa wagombea wawili; Lissu na Mbowe, wote waliwahi kuwa wabunge wa Singida Mashiriki na Hai. Mbali na ubunge na kushika nafasi mbalimbali ndani ya CHADEMA, Lissu pia aliwahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Uchaguzi ndani ya CHADEMA uliibua hisia na mambo mengi kwenye demokrasia ya Tanzania kwa zaidi ya mwezi mmoja tangu kuanza kampeni zao zilizosheheni minyukano baina ya wafuasi wa pande hizo mbili.
Uchaguzi huo uliohusisha nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti Bara na Tanzania Zanzibar, ulianza juzi Januari 21 na kukesha mpaka jana asubuhi, mshindi alipotangazwa.
Mapema juzi asubuhi, kwenye viwanja vya Mlimani City ulikofanyika uchaguzi huo, wajumbe pamoja wafuasi na wapambe wengine walifika wakiwa wanaimba nyimbo na kushangilia wakitaja jina la mgombea wanayemuunga mkono.
Hawakuishia kwenye nyimbo tu, wapo waliofikia hatua ya kushikana mashati wakati wa kutambiana wakiwa kwenye maeneo ya biashara za chakula na starehe ya karibu na Ukumbi wa Mlimani City ulikokuwa unafanyika uchaguzi huo.
Kwenye viwanja hivyo, nje ya ukumbi wa mkutano huo, mwandishi wa habari hii alishuhudia watu wengi, baadhi wakiwa wameketi kwa makundi wakifuatilia uchaguzi huo. Nyimbo za kejeli nazo zilikuwa sehemu ya uchaguzi huo.
Ndani ya ukumbi, chama hicho kiliweka walinzi maalum kutoka kampuni ya ulinzi kuzuia mtu yeyote asiyehusika kuingia ndani na katika kipindi chote cha upigaji kura, hakukuwa na mtu aliyeruhusiwa kutoka ukumbini.
Ulinzi uliimarisha hadi msalani, walinzi na wafuatiliaji maalum wa uchaguzi huo waliweka viti na kuketi pembeni ya milango ya kuingilia msalani na hawakuruhusu majadiliano yoyote kwa waliokwenda huko.
WALIVYONADI SERA
Moja ya hatua zilizoteka hisia za wajumbe katika uchaguzi huo ni namna wagombea walivyonadi sera zao, hata maswali yaliyoulizwa na kujibiwa.
Katika hatua hiyo, wajumbe walizuiwa kushangilia, kuzomea au kucheka, lakini wakati mwingine zuio hilo lilishindikana kutekelezwa, yote hayo yaliyopigwa marufuku, yakafanyika.
Wakati akiomba kura, Mbowe alitoa tahadhari kwa wajumbe kwamba wasibadili jenerali katikati ya vita. Alisisitiza kubadili jenerali katikati ya vita ni hatari kwa ustawi wa chama hicho.
Odero kwa upande wake, aliwaomba wajumbe wamchague ili awapatanishe Mbowe na Lissu na timu zao kwa kuwa minyukano imesababisha mafarakano ndani ya CHADEMA.
Naye Lissu alitumia dakika zake tano za kuomba kura, kukosoa hoja ya Mbowe ya "kutokimbilia kubadili jenerali katikati ya vita", akikumbusha madhila ambayo chama hicho kimepitia katika uchaguzi wa mwaka 2019, 2020 na 2024.
Lissu ambaye ni mtaalamu wa sheria, alisema kuwa mwaka 2019, CHADEMA haikushinda hata mtaa mmoja katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa; ikaambulia mbunge mmoja wa jimbo (kuchaguliwa na wananchi) katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na miezi miwili iliyopita imeambulia asilimia 0.8 ya mitaa na vijiji kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, lakini "jenerali yupo na hajafanya lolote kunusuru chama chake".
Ni kauli ambayo iliwafanya wajumbe kushindwa kuficha hisia zao, baadhi wakicheka, wengine wakimshangilia Lissu na wengine wakilaumu wasimamizi wa uchaguzi kwa kufumbia macho 'mashambulizi' ya Lissu kwa Mbowe.
Lissu alihitimisha hoja yake kwa kuwapa tahadhari wajumbe kwamba kwa kuzingatia mifano hiyo, walipaswa kuamua wamwongeze muda Mbowe aongoze kwa miaka 26 waendelee na madhila yaliyopo au wafanye mabadiliko kwa kumpa kura zao.
Kabla ya kupiga kura, kulifanyika uhakiki mkali wa wajumbe na kwa kipindi chote cha uchaguzi, wasimamizi walihakikisha unakuwa wazi, wajumbe wakiitwa kwa majina (wasiozidi sita) kwenda kupiga kura kwa kupeana nafasi na ilitolewa fursa kwa yeyote mwenye dukuduku au kuwa na taarifa yenye shaka, alipewa nafasi kueleza shaka yake na utatuzi wa utata kuhusu mjumbe husika ulifanyika hadharani.
Ni hatua iliyowezesha kubainika kuwapo wajumbe wachache ambao kikatiba hawakutakiwa kupiga kura hiyo au kutoka nje wakati wa shughuli hiyo inaendelea. Ilitolewa taarifa na wakaondolewa ukumbini.
Baadhi ya wajumbe wa uchaguzi huo, walipongeza namna utaratibu wa uchaguzi mwaka huu ulivyopangiliwa hususani katika eneo la kuufanya uwe wa wazi na kushuhudiwa na kila mtu aliyekuwa ndani na nje ya ukumbi.
UCHAGUZI WARUDIWA
Uchaguzi katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar ulirudiwa baada ya wagombea wote wanne waliokuwa wakigombania nafasi hiyo kushindwa kufikisha asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa.
Kutokana na uchaguzi huo kurudiwa, utangazaji matokeo yote haukufanyika mpaka pale ulipokamilika uchaguzi wote. Hata hivyo, wafuasi wa Lissu waliokuwa ndani ya ukumbi na nje, tayari walikuwa wamepata taarifa za matokeo. Hawakusubiri tangazo rasmi, walishangilia ushindi muda huo huo, hata ikamlazimu Mbowe naye kukosa uvumilivu, akatumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kuwapongeza Lissu na John Heche kwa kuchaguliwa kuongoza chama hicho.
"Nimepokea kwa mikono miwili uamuzi wa uchaguzi wa Mkutano Mkuu wa chama chetu cha CHADEMA uliohitimishwa leo (jana) asubuhi 22 Januari, 2025. Ninampongeza Mhe. Tundu Lissu na wenzake kwa kuaminiwa kutwikwa jukumu la uongozi wa chama. Ninawatakia kila la kheri katika kukipeleka mbele chama chetu," aliandika Mbowe.
Wagombea wawili ambao uchaguzi ulirudiwa kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Zanzibar, ni Said Mzee Said na Said Issa Mohamed ambao walipata kura zaidi ya wenzao wengine wawili.
Mbali na Mbowe, Mwenyekiti Kanda ya Victoria aliyekuwa anagombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Ezekia Wenje pia alikubali matokeo na kuwapongeza Lissu na Heche kwa ushindi.
"Our people have spoken: Ninakupongeza sana Mhe TL (Lissu) na ndugu yangu Heche kwa ushindi, tutawapa ushirikiano pamoja na check and balance. Kwa walioniunga mkono pamoja na campaign team yangu, Mungu awabariki sana. To Freeman Mbowe you are the icon of our democracy," aliandika Wenje.
WADAU WALONGA
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, alimpongeza Lissu kwa ushindi na kumwahidi ushirikiano wa dhati katika harakati za kuimarisha demokrasia nchini.
Kupitia chapisho lake katika mtandao wa X, Dorothy, aliandika: "Ninakupongeza Ndugu Tundu Lissu kwa kushinda uchaguzi na kuwa Mwenyekiti wa chama chako cha CHADEMA. Kuchaguliwa kwako kunakufanya pia uwe Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). Nikiwa Makamu wako huko, ninakukaribisha sana katika uongozi wa TCD.
"Nikiwa Kiongozi wa ACT Wazalendo ninakuhakikishia ushirikiano wa dhati katika kupigania demokrasia ya nchi yetu. Pia ninampongeza Mbowe kwa kukamilisha muda wake wa uongozi na kuonesha mfano wa ukomavu wa kisiasa."
Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alimkaribisha Mbowe katika maisha mapya ya kustaafu huku akimpongeza kwa mchango wake aliotoa kwenye siasa za mageuzi nchini.
"Ninakukaribisha Mwenyekiti mstaafu Mbowe katika ustaafu na kukuhakikishia kuwa kuna mengi ya kufanya nje ya siasa za uongozi katika kazi kubwa iliyo mbele yetu ya kujenga na kustawisha demokrasia ya nchi yetu ambayo inatuhitaji wana-mageuzi wote walio ndani na nje ya uongozi," aliandika Zitto.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED