KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimewahamasisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi, kuwekeza mkoani hapa, kutokana na uwapo wa mazingira mazuri.
Kadhalika, imebainishwa tayari yapo maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli hizo, kama vile Buzwagi Economic Special Zone, wilayani Kahama.
Mwenyekiti wa Bodi ya TIC, Dk. Binilith Mahenge, amesema hayo leo, wakati wa ziara mkoani hapa, kutembelea kiwanda cha uzalishaji mafuta ya kula cha Jielong Holding, kilichopo Nhelegani, manispaa ya Shinyanga.
Amesema TIC wapo ziara mkoani Shinyanga, kwa kutembelea baadhi ya miradi ambayo imesajiliwa na kituo hicho, ili kuona maendeleo yao pamoja na kubaini changamoto ambazo zinawakabili.
“Shinyanga ina mazingira mazuri ya uwekezaji, takwimu za mwaka 2023 ambazo TIC tulisajili miradi ilikuwa 500, lakini mwaka 2024 ilifika 901na mkoa huu unashika nafasi ya 10, kwa usajili wa miradi. Mwaka jana ilisajili miradi 16 kati ya mikoa 26 ya Tanzania bara,” amesema Dr.Mahenge.
“Hii inaonesha mkoa huu umeboresha mazingira mazuri ya uwekezaji, sababu kuna mahitaji yote muhimu ya kuvutia wawekezaji na wametenga maeneo, hivyo rai yangu kwa wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi, waje wawekeze hapa Shinyanga,” ameongeza.
Amewapongeza wawekezaji wa kiwanda hicho, kwa kuwekeza nchini na kutoa ajira kwa vijana, kuinua uchumi wa wakulima pamoja na serikali kupata mapato, akiwasihi wakulima wa pamba kuongeza kasi ya uzalishaji wa zao hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amesema mkoa huo una mazingira mazuri ya kuwekeza, ikiwamo miundombinu ya barabara, reli, uwanja wa ndege, umeme na maji ya kutosha.
“Tunakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza Shinyanga, sababu mahitaji yote yapo,” amesema Macha.
Msimamizi wa kiwanda hicho, Qi Liaoyuan, ambaye ni raia wa China, amesema kiwanda kilianzishwa mwaka 2012, kimetoa ajira na kina uwezo wa kuzalisha tani 150,000 za mbegu za pamba kwa ajili ya mafuta ya kula.
Amesema kwa sasa wamesimamisha uzalishaji wa mafuta hayo, mara baada ya kukosekana kwa malighafi ya mbegu za pamba na kwamba wanasubiri msimu uanze tena wa pamba ndipo waendelee na uzalishaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED