MWANAMKE ni mama, mzazi ambaye daima ni mlezi wa jamii.
Hivyo, katika nafasi yake anatakiwa kutambua anabaki kuwa mhimili mkubwa katika kupambana na kuimarisha gurudumu la maisha, hata likasonga mbele.
Kila analopitia mwanamke, humzunguka kila mtu likimhusu kwa namna moja au nyingine. Hivyo, wanawake wanapaswa kusimama kwa kuwaongoza wa toto wa kike, ili waweze kutambua nafasi yao na kujua ni kipi kinafaa na kisichofaa, kinachostahili na kisichostahili.
Kwa ujumla wanaangukia wajibu wa kufahamu mambo mtambuka yanayowazunguka.
Familia nyingi za Kiafrika zimekuwa na mtazamo tofauti kuhusu kinamama, wakiwapo wanaoamini nafais yake kuu ni “mfanyaji kazi za nyumbani.”
Kwa dhima waliojiwekea katika hilo, kuna matukio ya wanaume hao, hutumia fursa hiyo kuwatumikisha wake zao katika namna isiyofaa, wapo wanaofikia mbali kuwaletea magumu yasiyo na huruma.
Mfano kuna jamii wanaegemea mila kwamba, kinamama hawaruhusiwi kuwa na kauli sehemu yeyote, kwa kutoa hoja zake iwe katika ukoo au kaya mbalimbali.
Mwanamke huyo anashinda nyumbani akitekeleza majukumu yote, baadhi ya mikoa kuna wanaume wanaendelea kutumikisha kinamama, pasipo kujali ama wamechika au la.
Hapo mama huyo anaelemewa akikata kuni, kuchota maji, kupika na safari zisizikoma za shambani, ihali mwanaume akiwa amekaa, hoja yake kuu ‘yeye ndiye muoaji.’
Kuanzia nukta hiyo niliyoishia, kwa uchungu natamka ujumbe huu “
Wanaume, peaneni elimu, mkumbuka kuwa mwanamke ana haki, kwani hata yeye anachoka, hivyo anatakiwa kupumzika.”
Hilo ni jambo linalosaidia kuweka usawa kwa wote, wakipeana elimu, juu ya kurithi, siyo suala la mwanamke kuangukia tena mila za baadhi ya makabila wao wakirithi wajane.
Hilo linatokea, pasipo ridhaa zao. Ni muhimu kutambua kua huo ni unyanyasaji na ni makosa kisheria kumgandamiza haki na uhuru wa mwanamke, hivyo ni vyema mkaacha mila hizo.
Mwanamke katika hilo namhimiza kokote aliko, suala hilo la mjane kurithiwa na ndugu limepitwa na wakati.
Nawatia moyo wanawake wenzangu, wajikwamue katika hilo, kwani sheria zipo za kuepuka ukatili huo.
Hivyo, mwanaume uliyemrithi mjane chukua hatua kwani sio vyema kumuweka mtu kifungoni kwani anakosa uhuru wa kuongea lolote.
Mwanamke anayo nafasi kubwa katika jamii, anao uhuru wa kushiriki kwenye siasa wakati tunaingia mwaka 2025 wa uchaguzi mkuu.
Hivyo inatupasa kukumbuka kuwapo nafasi ya kuwa wazalendo, tukishiriki kikamilifu kwenye uchaguzi na kuwa wenye maono ya kuwania cheo chochote.
Nanyi kinamama, msiache kuwa na malengo ya kutimiza ndoto zenu, kwani kuna baadhi ya wazazi vijijini wamekuwa na mtazamo tofauti katika malezi ya watoto.
Ninaamini, mtoto hawezi ana haki. Wako sawa katika jamii, huku akiwa na uwezo wa kumsaidia kila mtu.
Pia, tusisahau kuwa, mtoto wa kike anaweza kuikomboa dunia, ni mama wa jamii, pale anapopewa haki, anakuwa na uthubutu wa kukomboa taifa zima.
Tujue, watu wote wapewe elimu kua mtoto wakike ni chanzo cha maendeleo na inatupasa kuvikumbuka yombo vinavyotetea haki za wanawake vipo.
Kisiasa nako bado hakuko juu sana, ingawa kwetu Tanzania tuna walau rekodi nzuri, tunaye Rais Samia Suluhu Hassan, huku jana tulisikia chama cha ACT Wazalendo, nacho kaibuka
Mwanamama Dorothy Semu, katangaza kuingia kinyang’anyiro cha chama chake, kuwania kupeperusha bendera ya chama chake, akiwania urais.
Bila shaka watoto wa kike walioko shuleni, wana wajibu wa kusoma kwa bidii wakiwa nafasi ya juu zaidi, kuongoza katika fursa mbalimbali.
Bila kusahau kinababa wote, nao wapeane elimu juu ya utambuzi wa nafasi ya mtoto wakike na wakina mama kwa ujumla, taifa letu litazidi kuwa imara zaidi.
Niwasihi wanaume wapeni fursa kinamama msiwabane kwani wanayo nafasi kwenye ngazi za familia na kisiasa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED