LEO Yanga ina kibarua kigumu na muhimu cha kusaka pointi tatu muhimu za kuwapeleka hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa namna msimamo wa kundi A wa michuano hiyo, Yanga ina kila sababu ya kupata ushindi ili kufuzu kwa mara ya pili mfululizo hatua hiyo ya robo fainali.
Yanga ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi saba chini ya wapinzani wao wa leo MC Alger wenye pointi nane huku Al Hilal wakiongoza kundi wakiwa na pointi 10, hizo zote ni kabla ya michezo ya leo.
Kutokana na hilo, MC Alger nao wamejipanga na wamejiandaa kikamilifu kwa ajili ya mchezo wa leo kwani wanafahamu umuhimu wa ushindi kwa kuweza kutinga robo fainali.
Hata hivyo kimahesabu ni kama Waarabu hao wana machaguo mawili kwenye matokeo ya leo, sare yoyote kwao ina faida na watakuwa wamefuzu moja kwa moja kucheza robo fainali.
Ugumu wa mchezo wa leo unawafanya Yanga kutoingia uwanjani wakiwa na matokeo yao kichwani, wanapaswa kuingia kwa tahadhari na kupambana kwa muda wote kuweza kupata ushindi utakaowapeleka robo fainali.
Wachezaji wafahamu mashabiki wao wapo nyuma yao, kitu pekee cha kufanya ni kuhakikisha wanapambana muda wote ndani ya uwanja na kucheza kwa tahadhari kubwa kwa sababu hawana chaguo lingine zaidi ya ushindi tu.
Matokeo zaidi ya ushindi yatawafanya msimu huu kuishia hatua ya makundi kitu ambacho si malengo yao na hata mashabiki wao watahuzunika sana hasa baada ya kuona wapinzani na watani zao wa jadi, Simba wakitinga robo fainali ya michuano Kombe la Shirikisho Afrika.
Utamaduni wa soka letu, Simba na Yanga ni watani ambao kila mmoja anaombea mwenzake asifanikiwe ili wapate nafasi ya kuchekana na kutaniana na kunogesha soka letu.
Mpaka sasa katika Kombe la Shirikisho Afrika, Simba yenyewe tayari imeshajihakikishia kucheza robo fainali, kesho itaingia uwanjani kucheza na CS Costantine kusaka nafasi ya kuongoza kundi lao.
Yanga wamepoteza nafasi ya kuongoza kundi lao, lakini bado wana nafasi ya kufuzu robo fainali kama tu watafanikiwa kupata ushindi kwenye mchezo wa leo dhidi ya wapinzani wao MC Alger.
Yanga wana nafasi ya kufikia hatua hiyo, lakini lazima wajipange uwanjani, wacheze kwa nidhamu kubwa, wawanyime nafasi wapinzani wao kumiliki mpira.
Tunataka kuikumbusha Yanga tabia za Waarabu katika hatua kama hizi wanapowania nafasi ya kusonga mbele hasa wanapokuwa ugenini, kama watafanikiwa kupata goli la kuongoza watacheza mpira wa kupoteza muda.
Lakini watataka kucheza zaidi na mwamuzi kwa maana ya kulalamika sana, watacheza mpira wa taratibu na kupoteza muda sana kwa kujiangushaangusha.
Ili kuyaepuka haya yote, Yanga wanapaswa kuchanga karata zao vizuri kwa kuhakikisha wanaanza wao kupata bao na kuhimiri kasi yao Waarabu wanapotafuta bao, hakuna kinachoshindikana.
Nipashe tunazitakia kila la heri klabu zetu zote, Yanga kutinga robo fainali na Simba kupata ushindi utakaowafanya kuingia robo fainali wakiwa wanaongoza kundi lao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED