TCRA yaonya wasiozingatia masharti utangazaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:05 AM Jan 18 2025
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari.
Picha: Mtandao
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari.

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeonya watoa huduma za utangazaji wanaokiuka vipengele kadhaa vya kanuni za utoaji maudhui kuwa itaendelea kuwachukulia hatua stahiki za kiudhibiti na kiusimamizi.

Taarifa ya hali ya mawasiliano Tanzania iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari, jijini Dar es Salaam jana, inaonesha maeneo ya ukiukwaji yaliyothibitishwa baada ya ufuatiliaji wa maudhui ya televisheni 16 na redio 12 zenye leseni za kitaifa kati ya Oktoba na Desemba, mwaka jana. 

“Maeneo ambayo watoa huduma wengi wa televisheni wamekiuka ni kwenye uzingatiaji wa ratiba ya vipindi, dakika zinazotakiwa kwa taarifa ya habari," alisema.  

Alisema utaratibu wa TCRA wa maombi ya leseni za maudhui ya redio na televisheni unawataka waombaji kueleza jinsi watakavyohakikisha ubora wa vipindi, faida za  vipindi kwa uchumi wa jamii. Pia wanatakiwa kuwasilisha ratiba ya vipindi kabla ya kuanza kuvitoa na kuizingatia. Ratiba inatakiwa kueleza muda, mpangilio na idadi ya vipindi.

Taarifa hiyo ya TCRA inaonesha kuwa televisheni sita kati ya 16 zilizotathminiwa zilizingatia ratiba iliyowasilishwa Mamlaka mapema. Hii ni pamoja na kuwa 12 kati ya hizo ziliwasilisha ratiba.

Watoa huduma wamefanya vizuri kwenye utoaji wa maudhui ya ndani, ambapo kanuni zinataka yawe angalau asilimia 60 na kwenye vipindi vya elimu.  

Hata hivyo, matokeo ya ufuatiliaji huu yanaonesha mabadiliko kulinganisha na Septemba 20254 ambako redio zote 12 zilizopitiwa zilikiuka masharti ya kuzingatia ratiba. 

Huduma za televisheni zinatolewa kupitia mitambo iliyosimikwa ardhini (DTT), kwa njia ya madishi ya setelaiti (DTH) na kwa waya. Mifumo ya DTT na DTH inahitaji visimbuzi ambavyo vinapokea maudhui na kuyawezesha kuonekana kwenye televisheni. Takwimu zinaonesha kuwa Desemba 2024 kulikuwa na visimbuzi 2,148,763 vilivyolipiwa vifurushi.

Kampuni tano zina leseni za kutoa huduma za kusambaza maudhui kupitia ving’amuzi. Hizo na idadi ya visimbuzi vya mfumo wake kwenye mabano ni Azam TV (1,340,135),  Star Media (477,527), Multichoice Tanzania (225,263), Agape Associates (1,840), Basic Transmission – Digitek (15,000), Continental (67,663) na Wananchi Cable (21,335).

Azam Media Limited ina idadi kubwa ya visimbuzi vya DTT vilivyolipiwa vifurushi ikilinganishwa na watoa huduma wengine, ikifuatiwa na Star Media Limited. Kwa ujumla, idadi ya visimbuzi vya DTH vilivyolipiwa vifurushi ni vingi kuliko visimbuzi vya DTT.

Idadi ya televisheni zinazopokea maudhui kwa njia ya waya iliongezeka kutoka 15,781 Machi 2024 hadi 16,767 Desemba 2024. Shinyanga inaongoza kwa kuwa na 4,219, ikifuatiwa na Mwanza (2,070) na Tabora (1,872).