Kikongwe mwenye umri wa miaka 62, Asha Mayenga, mkazi wa Mtaa wa Lugela, Kata ya Nyahanga, Manispaa ya Kahama, ameuawa kikatili na watu wasiojulikana, kisha mwili wake kufukiwa shambani katika Kijiji cha Malindi, Kata ya Busoka, alikokuwa amekwenda kupanda mpunga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, alithibitisha tukio hilo na kusema marehemu alipotea tangu Januari 13, 2025, na mwili wake ulipatikana Januari 17, ukiwa na majeraha ya kupondwa kichwani. Polisi wanawashikilia watu watatu, akiwemo mtoto wa marehemu, kwa ajili ya upelelezi zaidi.
Magomi amesema uchunguzi wa awali umebaini mgogoro wa ardhi kati ya marehemu na mtoto wake, na aliwasihi wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi. Aliongeza kuwa mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa familia kwa maziko baada ya kufukuliwa na kufanyiwa uchunguzi. Tukio hilo liliripotiwa na mchungaji wa ng'ombe aliyegundua harufu kali eneo la tukio.
Mume wa marehemu, Mashauri Mlekwa, ameeleza kuwa mnamo Januari 13 alipata taarifa kutoka kwa mjukuu wake kwamba bibi yao hakuweza kurejea nyumbani baada ya kutoka shambani na vijana wawili, ambao walidai walimwacha nyuma. Familia ilianza kumtafuta bila mafanikio, na siku iliyofuata waliripoti polisi.
Mnamo Januari 16, Mlekwa alipata taarifa kutoka kwa mfugaji kwamba eneo la shamba lilikuwa likitoa harufu mbaya, na baada ya kufika, walibaini uwepo wa mwili uliozikwa. Polisi, wakiwa na daktari, walifukua mwili huo mnamo Januari 17 na kuthibitisha kuwa ni wa Asha Mayenga.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Seke, Christopher Robert, amesema tukio hilo ni la kikatili na halijawahi kutokea mtaani hapo. Amewataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kusisitiza adhabu kali kwa wahusika ili iwe fundisho.
Mmiliki wa mifugo jirani na eneo la tukio, Juma Dutu, amesema mifugo yake ilipokaribia shamba la marehemu, ilikimbia, hali iliyowafanya vijana wake kupata hofu. Alimjulisha mume wa marehemu, na baada ya uchunguzi, mwili wa bibi huyo ulibainika kuwa umeharibiwa vibaya.
Kamanda Magomi alisisitiza kuwa mauaji hayo ni ya kikatili na yanaonyesha dharau kubwa kwa utu wa binadamu. Ameahidi uchunguzi wa kina na hatua kali kwa wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED