Serikali kuendelea kuhifadhi machapisho yote TLSB

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 03:21 PM Jan 17 2025
Picha wakati wa ufunguzi wa mkutano wa waandishi na wachapishaji wa vitabu ulioandaliwa na Bodi ya Taifa ya  Huduma za Maktaba Tanzania TLSB.
Picha: Mpigapicha Wetu
Picha wakati wa ufunguzi wa mkutano wa waandishi na wachapishaji wa vitabu ulioandaliwa na Bodi ya Taifa ya Huduma za Maktaba Tanzania TLSB.

SERIKALI kupitia Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), imesema itaendelea kuhifadhi machapisho ya vitabu vya ajili ya kukuza maarifa na elimu kupitia vitabu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Hayo yalisemwa  jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya TLSB,   Profesa Rwekaza Mukandala, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wachapishaji na waandishi wa vitabu.

Mkutano huo wa siku mbili wa wachapishaji na waandishi wa vitabu uliandaliwa na bodi ya huduma za maktaba Tanzania na kufanyika kwenye ofisi za Maktaba Kuu ya Taifa jijini Dar es Salaam.

Ametaja mada mbili zilizojadiliwa kuwa ni utekelezaji wa sheria ya amana kwenye maktaba mtandao  jumuishi ya taifa na umuhimu wa ununuzi wa vitabu kwaajili ya ukuzaji wa soko la ndani.

Profesa Mukandala amesema Sheria ya amana  ya mwaka 1975 inasisiza umuhimu machapisho yote yanayochapishwa ndani ya nchi kuhifadhiwa kwenye maktaba kuu ya taifa ili kulinda na kuhifadhi urithi wa kitamaduni na kiakili kwaajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Amesema TLSB inatoa jukwaa la kidijitali ambalo linarahisisha uhifadhi, upatikanaji na usambazaji wa machapisho hayo kwa watumiaji wa ndani na nje ya nchi.

“Hii ni fursa kubwa kwa waandishi na wachapishaji wa vitabu katika kuweka hazina ya maarifa na kutambulisha kazi za ndani kimataifa na katika hilo tunapenda kusisitia ushirikiano wa karibu kati ya TLSB na wadau ili kuhakikisha machapisho yenu yanawafikia wadau wengi,” amesema

Kuhusu ununuzi na matumizi ya vitabu vya ndani, Profesa Mukandala amesema Serikali kupitia TLSB imejidhatiti kuunga mkono waandishi na wachapishaji wa ndani kwa kununua vitabu vingi vya ndani vyenye maudhui ya kitanzania.

“Katika mwaka huu wa fedha 2025/2026 serikali kupitia TLSB imeweka bajeti kubwa katika ununuzi vitabu na machapisho ya ndani hatua ambayo itaongeza hamasa kwa waandishi na wachapishaji wengi wa Tanzania kushriki katika mchakato wa kukuza maarifa na elimu,” amesema na kuongeza

“Nawahimiza washiriki kutumia mkutano huu kama jukwaa la kujadili fursa zinazotokana na utekelezaji wa sheria ya amana na mchakato wa ununuzi wa vitabu itakayotolewa na watoa mada, mawazo yenu ni muhimu kuboresha kazi zetu na kuinua soko la vitabu hapa nchini,” amesema Mukandala.

Amesema TLSB itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali nchini katika utekelezaji wa sheria ya amana ili kuwezesha fani kuwa nguzo muhimu ya maendeleo hasa katika kusukuma maendeleo ya taifa  kwa kutumia maktaba jumuishi mtandaoni katika kukuza uchumi wa kidijitali.

“Maktaba jumuishi kitaifa mtandaoni inakwenda kuruhusu upatikanaji wa vitabu vingi kidijitali na usajili wa vitabu utafanyika mtandaoni kwa hiyo mfumo utarahisisha usambazaji wa vitabu na utasaidia soko la ndani na kukuza uchumi kupitia mabadiliko makubwa ya teknolojia,” amesema