DC akerwa fedha za wananchi kushindwa kutumika kupaua zahanati

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 06:49 PM Jan 16 2025
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akisikiliza kero za wananchi wa kijiji cha Mwang'halanga na kuzitatua.
Picha:Marco Maduhu
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akisikiliza kero za wananchi wa kijiji cha Mwang'halanga na kuzitatua.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, ameonyesha kukerwa na kitendo cha kushindwa kupaua zahanati ya Kijiji cha Mwang’halanga licha ya wananchi kuchangia Shilingi milioni 11.7 kwa kazi hiyo, huku sababu ikielezwa kuwa ni kukwama kwa mfumo wa manunuzi wa kielektroniki (NeST).

Mtatiro alionyesha masikitiko yake jana wakati wa mkutano wa hadhara kijijini hapo, ambao ulikuwa ni sehemu ya ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.

“Haiwezekani wananchi wachange Shilingi 28,000 kila kaya, jumla ya Kaya 418 wakafanikisha Shilingi milioni 11.7 kwa ajili ya kupaua zahanati yao, halafu mnakuja kuniambia eti haijapauliwa kwa sababu ya mfumo wa NeST. Acheni mchezo na pesa za wananchi. Nawaagiza ifikapo tarehe 27 mwezi huu zahanati hii iwe imepauliwa, na nitakuja mwenyewe na kamati yangu ya ulinzi na usalama kuhakikisha hilo limetekelezwa. Ole wenu nikute hakuna kitu,” alisema Mtatiro kwa ukali.

Hata hivyo, Mtatiro alimpongeza Mtendaji wa Kijiji cha Mwang’halanga, Helena Kayagila, kwa kuweka fedha hizo kwenye akaunti ya kijiji kwa uaminifu. Alisema sehemu nyingine fedha kama hizo zingekuwa tayari zimeshatumika vibaya. Helena alihifadhi pia Shilingi milioni 3 zilizotolewa kupitia mfumo wa jimbo, hivyo kufanya jumla ya fedha zilizopo kufikia Shilingi milioni 14, kama inavyoonyeshwa kwenye risiti za benki.

1

Helena, alipoulizwa kuhusu kuchelewa kwa upauaji wa zahanati hiyo, alisema michango ya wananchi ilichangwa tangu Agosti mwaka jana na kuhifadhiwa kwenye akaunti ya kijiji. Hata hivyo, juhudi za kupaua zahanati hiyo zilikwama kutokana na mfumo wa manunuzi ya umma wa kielektroniki (NeST).

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Edward Maduhu, alithibitisha kuwa fedha hizo zipo salama, lakini mradi huo haukuingizwa kwenye mfumo wa NeST, jambo lililokwamisha utekelezaji wake.

Baadhi ya wananchi wa Mwang’halanga, akiwemo Manase Elias, walieleza kuwa endapo fedha zao zimeshindwa kutumika kama ilivyokusudiwa, ni bora zirudishwe kwao. Walisisitiza kuwa walichangia fedha hizo kwa lengo la kupata huduma za matibabu karibu na makazi yao, lakini wanahofia fedha hizo zimetumika vibaya.

Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya pia alisikiliza changamoto mbalimbali za wananchi, zikiwemo ukosefu wa maji, ubovu wa barabara, kutokamilika kwa maboma ya zahanati, ukosefu wa umeme, na migogoro ya ardhi. Alitoa agizo kwa wazazi wote kuhakikisha watoto wao wanarudi shule mara moja, akisema baada ya Ijumaa ya leo, zoezi la ukamataji wa wazazi wasiotekeleza agizo hilo litaanza rasmi.