Kwa mara ya kwanza, Tanzania inatarajia kuanzisha tuzo za kutambua na kuthamini mchango wa wasanii katika tasnia ya vichekesho (uchekeshaji) chini ya usimamizi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Bodi ya Filamu kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Tuzo hizo, zitakazokuwa na jumla ya vipengele 17, zinatarajiwa kutolewa Februari 14, 2025, katika ukumbi wa SuperDom, Masaki jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tuzo hizo, mwanzilishi wa wazo hilo, Omary Nyembo maarufu kama Ommy Dimpoz, alisema tuzo hizo zitaleta chachu ya maendeleo katika tasnia ya uchekeshaji, kuongeza ajira kwa vijana, na kupunguza utegemezi.
“Tunatambua mchango wa waanzilishi wa tasnia ya uchekeshaji ambao wamekuwa kiini cha kuvutia vijana wengi kuingia katika fani hii. Hawataachwa nyuma katika tuzo hizi,” alisema Ommy Dimpoz.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa BASATA, Dk. Kedmon Mapana, aliahidi kuwa tuzo hizo zitasimamiwa kwa weledi ili kuhakikisha zinafanikiwa kitaifa na hata kimataifa.
“BASATA itahakikisha tunasimamia kwa uadilifu mkubwa ili kusiwe na changamoto zozote. Tutaweka mfumo wa haki na uwazi kwa kila mshiriki,” alisema Dk. Mapana.
Aidha, Dk. Mapana alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inaunga mkono wasanii wa aina zote bila ubaguzi, na kuwataka vijana kuchangamkia fursa hii.
“Tuzo hizi ni fursa ya pekee kwa sekta ya sanaa kupiga hatua kubwa zaidi, kuongeza ajira, na kuchangia katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” aliongeza.
Tuzo hizi zinalenga kuongeza thamani ya sanaa ya uchekeshaji nchini na kuweka msingi wa heshima na kutambua juhudi za wasanii waliobobea na chipukizi katika tasnia hiyo.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Dk. Gervas Kasiga, alitangaza vipengele 17 vya tuzo hizo, ambapo washindi wa tuzo tatu kubwa watajinyakulia zawadi za fedha kama ifuatavyo:- Mchekeshaji Bora wa Kike atapewa zawadi ya shilingi milioni 20, Mchekeshaji Bora wa Kiume atanyakua shilingi milioni 20 na Mchekeshaji Bora wa Mwaka atabeba shilingi milioni 30.
Aidha, washindi wa vipengele vingine vya tuzo watapata zawadi ya shilingi milioni 5 kila mmoja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED