JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata askari wawili wa usalama barabarani (trafiki) kwa tuhuma za kupokea rushwa kutoka kwa madereva wa mabasi ya abiria, maarufu kama daladala.
Jana katika mitandao ya kijamii ilisambaa video ikionyesha askari hao wakipokea kinachodaiwa kuwa ni rushwa kutoka kwa madereva na makondakta wa daladala waliowasimamisha kutokana na makosa ya kukiuka sheria za usalama barabarani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro, alisema askari hao, Koplo John na WP Koplo Mgisi, wameshawaakamata na kwa sasa wako mahabusu.
Alisema hatua za kinidhamu za mashtaka ya kijeshi zimeshaanza kuchukuliwa dhidi yao wakati wakisubiria hatua zingine za kisheria.
Kamanda Muliro alisema wakati askari hao wakitekeleza majukumu yao, walifanya vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha maadili, hivyo kuchafua taswira ya Jeshi la Polisi na serikali.
"Askari hawa tayari wamekamatwa, wako mahabusu na hatua kali za kinidhamu za mashtaka ya kijeshi zimeanza kuchukuliwa, " alisema.
Kwa mujibu wa Muliro, jeshi hilo litaendelea kuchukua hatua kali na za haraka na halitavumilia vitendo vyovyote vya kulidhalilisha au vilivyo kinyume cha maadili ya jeshi hilo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED