Mahakama yamwonya mtoto wa Mbowe

By Kulwa Mzee , Nipashe
Published at 12:00 PM Jan 15 2025
Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe.
Picha: Mtandao
Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe.

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Kazi imemwonya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe kwa kutofika mahakamani tangu shauri la madai ya malimbikizo ya mishahara ya waandishi wa habari 10 lilipofunguliwa na imemwamuru kulipa fedha hizo.

Dudley ambaye ni mtoto wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe alipewa amri hiyo jana mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mary Mrio wakati shauri hilo la madai lilipokuwa linatajwa.

Msajili Mrio alisema shauri hilo liliitwa jana kwa ajili ya kuangalia maombi ya waandishi wa habari ya kumkamata Dudley kuwa mfungwa wa kiraia kwa kushindwa kulipa malimbikizo ya mishahara yao.

Alisema maombi hayo hayajawasilishwa, hivyo aliamuru ndani ya siku saba yawe yamewasilishwa mahakamani kwa ajili ya kupangiwa Jaji wa kuyasikiliza.

Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Dudley, Samadani Mngumi alidai hajazungumza na mteja wake zaidi ya kupokea maelekezo ya kufika mahakamani kuomba udhuru hadi Januari 28 aweze kufika.

Msajili Mrio alihoji kwamba anafika mahakamani kulipa au mazungumzo tu na kwamba tangu shauri hilo liwapo hajawahi kuhudhuria.

"Mteja wako ameitwa mara kadhaa, hajawahi kufika mahakamani na hata simjui na sijawahi kumwona, afike mahakamani awe amelipa," alisema.

Shauri liliahirishwa hadi Januari 31 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa maombi ya kumkamata mkurugenzi huyo ambayo yanatakiwa kuwa yamewasilishwa ndani ya siku saba kuanzia jana.

Awali mahakama ilitoa amri ya waandishi hao kulipwa baada ya kupitia hoja za washinda tuzo katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Julai 2023.

Shauri hilo namba 28461 la mwaka 2023, wadai ni Maregesi Paul na wenzake tisa dhidi ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe.

Walalamikaji hao walipata tuzo Julai 17, 2023 mbele ya Msuluhidhi wa CMA Ilala,  Bonasia Mollel.

Madai ya awali yalikuwa jumla ya Sh. milioni 114. Baada ya kukaa mezani kwenye majadiliano kwa pamoja kiwango hicho cha fedha kilishuka na kufikia Sh. milioni 62.7.

Dudley alikubali kulipa fedha hizo kwa awamu tatu, Oktoba 30, Desemba 30 mwaka 2023 na awamu ya mwisho ilikuwa mwishoni mwa Februari mwaka jana, lakini hakulipa.

Dudley aliingia makubaliano ya kulipa malimbikizo hayo nje ya mahakama Aprili hadi Mei mwaka jana, lakini hajafanya hivyo.