SHAHIDI wa upande wa Jamhuri, Sajenti Chedy amedai mahakamani kwamba hajui washtakiwa katika kesi ya kusafirisha kilogramu 15.8 za dawa za kulevya aina ya heroine walikamatwa lini.
Shahidi alidai hayo jana Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu Mahakama ya Mafisadi, mbele ya Jaji Monica Otaru wakati anajibu maswali ya Wakili wa Utetezi, Marietha Mollel.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni raia wa Nigeria, Nyebuche Ernest na mwenzake Henry Ogwanyi ambaye alifariki Dunia kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa Mahakama ya Mafisadi.
Katika kesi hiyo, mshtakiwa alibakia mmoja, Nyebuche, anayewakilishwa na Wakili Marietha anayesaidiana na Alfred Ahonga.
Akijibu maswali ya Wakili Marietha, shahidi huyo alidai hakumbuki sheria gani ilimwongoza kufunga vielelezo na hajui washtakiwa walikamatwa lini kwa sababu kazi yake ilikuwa kufunga kielelezo na kukabidhi tu.
Alidai kuwa kabla hajafunga vielelezo na kuweka alama, havikuwa na alama yoyote na katika vielelezo alivyooneshwa, hakuona gari wala picha ya aina yoyote.
Shahidi alidai alifunga vielelezo Aprili 21, 2019 saa 5.50 asubuhi hadi saa 10 jioni na Aprili 23, 2019 akiwa na Inspekta Msaidizi wa Polisi Philemon walipeleka vielelezo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi.
Alipohojiwa kama walikuwa na vyeti vya ukalimani, shahidi alidai hana pia hajui kama Inspekta Msaidizi Philemon anacho au la.
Alidai ushahidi wote aliotoa ndio sahihi kwamba baada ya kufunga vielelezo washtakiwa na shahidi huru waliandika majina yao na kutia saini, hoja kwamba mshtakiwa hakutia saini bali sahihi yake ilitengenezwa si sahihi.
Katika ushahidi wake awali, shahidi huyo alidai Aprili 21, 2019 alifunga vielelezo ambavyo ni pakiti sita zilizobainika kuwa dawa za kulevya. Alidai kazi yake ilikuwa kufunga vielelezo na kukabidhi kwa Inspekta Msaidizi Philemon.
Alidai kuwa wakati wa kufunga vielelezo, walitumia lugha ya Kiingereza na Kiswahili na walipofika kwa Mkemia, Inspekta Msaidizi Philemon ndiye aliyekidhi vielelezo kwa ajili ya uchunguzi.
Shahidi alipotakiwa kutambua washtakiwa, alidai anamtambua mshtakiwa Henry lakini hakuwa mahakamani na akamtambua mshtakiwa Nyebuche ambaye alikuwa kizimbani.
Washtakiwa wote wanadaiwa kuwa mwaka 2019, maeneo ya Kariakoo, jijini Dar es Salaam, walikutwa wanasafirisha dawa za kulevya aina ya heroine kilo 15.8.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED