Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma, amewataka waandishi wa habari kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi na zisizoegemea upande wowote kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 wa kuchagua madiwani, wabunge na rais.
Mwinjuma ametoa wito huo leo, Februari 14, 2025, wakati akihitimisha mkutano wa mwaka wa vyombo vya utangazaji nchini ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) jijini Dodoma. Mkutano huo wa siku mbili umelenga kuboresha sekta ya utangazaji na kuimarisha weledi wa waandishi wa habari.
"Vyombo vya habari vina nafasi kubwa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Msipotoa taarifa sahihi, mnaweza kuchangia demokrasia kuzama," amesema Mwinjuma.
Amesisitiza umuhimu wa waandishi kutumia lugha fasaha ya Kiswahili ili kuilinda na kuhakikisha haipotoshwi. Pia, amewahakikishia waandishi kuwa serikali inaunga mkono sekta ya habari na milango ya Wizara ipo wazi kwa ushirikiano.
“Dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuikuza sekta hii, ndiyo maana alipoingia madarakani alivifungulia vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa,” ameongeza Mwinjuma.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka, amewataka waandishi wa habari kuwa waangalifu wanaporipoti habari za uchaguzi na kuepuka kuongeza "chumvi." Pia, amesisitiza uwiano sawa wa muda wa vipindi kwa wagombea ili kuimarisha haki na demokrasia.
Mkutano huo ulihadhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya habari na utangazaji, huku kaulimbiu yake ikiwa "Wajibu wa Vyombo vya Utangazaji Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025."
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED