Mbunge wa Vwawa (CCM), Japhet Hasunga, amemsifu Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya katika kuleta maendeleo nchini, akisisitiza kuwa ni kiongozi shupavu anayehakikisha Tanzania inapiga hatua.
Akizungumza bungeni wakati wa kuchangia hoja, Hasunga alipendekeza kuwa Afrika iungane na kuwa taifa moja ili kuimarisha uchumi na kupunguza umasikini.
"Kama Afrika ikiungana na jinsi ambavyo Rais Samia anasimamia upatikanaji wa nishati safi, itasaidia sana kupunguza umasikini wa Watanzania," alisema Hasunga.
Mbunge huyo alisisitiza kuwa upatikanaji wa umeme na nishati safi utasaidia kuinua uchumi kwa kuongeza fursa za ajira na kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, alimpongeza Rais Samia kwa juhudi zake za kulinda afya za wanawake kwa kuhimiza matumizi ya nishati safi, pamoja na kusimamia ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) inayotumia umeme unaozalishwa ndani ya nchi.
"Ni mabadiliko makubwa. Tukifikia hatua ya kutumia nishati safi kwa upishi, tutakuwa tumepunguza gharama za fedha za kigeni ambazo sasa zinaweza kuelekezwa kwenye miradi mingine ya maendeleo," aliongeza Hasunga.
Mbunge huyo pia alieleza kuwa ana imani kubwa na uzalendo wa Rais Samia, akisema kuwa kutokana na utendaji wake bora, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM walikubaliana kwa kauli moja kuwa anafaa kuendelea kuongoza kwa miaka mingine mitano.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED