Makandarasi watakiwa kutumia wataalamu katika shughuli za ujenzi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:43 PM Feb 14 2025
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) Mhandisi Rhoben Nkori.
Picha: Mpigapicha Wetu
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) Mhandisi Rhoben Nkori.

Makandarasi wamehaswa kuhakikisha wanawatumia wataalamu stahiki katika utekelezaji wa shughuli za miradi ya ujenzi nchini.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo yaliyofanyika kwa siku tatu jijini Arusha, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) Mhandisi Rhoben Nkori alisema kuwa lengo ni  kukuza uwezo na ujuzi wa makandarasi wazawa kwa kutambua umuhimu wa usimamizi wa rasilimali mahala pa kazi za ujenzi (Resource Management in Construction Site).

"Naimani mmejifunza vitu vingi muhimu hasa kwenye kwenye resource Management na kazi iliyobaki sasa ni utekelezaji, lakini najua mnafahamu kuwa kwenye ujenzi rasilimali zipo kiasi gani na endapo zisipo simamiwa vizuri madhara yake huonekana mara moja, pia zipo negative impacts zinazokuja kuonekana baadae na madhara yake huwa ni makubwa kuliko zile resources ambazo impact yake inaonekana hapo hapo" alisema Mhandisi Nkori.

Pamoja na hayo alisema kuwa, ni wajibu wa makandarasi wote nchini kuhakikisha wanawatumia wataalamu stahiki ili kufanya kazi na kusimamia mikataba waliyoingia kwa viwango stahiki.

“Tunakutaka Mkandarasi uwe full package, ili uweze kusimamia rasilimali zote ulizonazo, mkataba wako wa kazi na baada ya hapo kujua unaenda kutekeleza nini kwa kutumia rasilimali zenye sifa stahiki”, alisema Mhandisi Nkori.

Sambamba na hayo, alitumia fursa hiyo kuwataka makandarasi kutoa taarifa za makandarasi wasiotumia wataalamu husika na kutaka kufanya kazi wao wenyewe bila kushirikiana na wataalamu stahiki.

"Endapo mkandarasi mzawa akiharibu kazi yeyote ile kwa kujenga chini ya viwango, makandarasi wazawa wote wanachafuka" alisema Mhandisi Nkori.

1

Aidha alibainisha kuwa, Bodi ya Usajili Makandarasi (CRB) inampango wa kuwa na Kampuni za ukandarasi ambazo zitakuwa zinatumia wataalamu husika kwa mda unaostahili. 

Baadhi ya Makandarasi waliohudhuria mafunzo hayo walisema wamepata fursa ya kujifunza kuwa wanaposhirikiana na wataalamu wanaongeza ufanisi wa kazi na faida kwa makandarasi.

Kwa upande wake Zephania Kwayu, mshiriki wa mafunzo hayo akitokea Kampuni ya Zekwa Trading Company LTD alisema kuwa, ushiriki wake kwenye mafunzo umemsaidia kuimarika katika eneo la usimamizi mzuri wa rasilimali mahali pa kazi za ujenzi ili kuhakikisha mradi unatekelezwa na kukamilika kwa ubora unaotakiwa.

“Nimefarijika na kufurahia kuhudhuria katika mafunzo haya, tumepata mafunzo mazuri, tumekuwa na mijadala mizuri na tumeweza kushirikishana uzoefu baiana ya makandarasi tuliohudhuria. Wakati mwingine tulidhani tunajua lakini kupitia mafunzo haya tumejua mengi zaidi” alisema Kwayu.

Aidha, aliishukuru Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) kwa uratibu wa mafunzo hayo na kuwataka makandarasi wengine kuhudhuria mafunzo yanayotangazwa na Bodi kwa ustawi wa tasnia ya Makandarasi. 

Naye, Grace Mungunasi alisema kupitia mafunzo hayo yamemsaidia kuyapata majibu ya changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza katika upande wa usimamizi wa rasilimali pa kazi za Ujenzi ambazo amekuwa akikumbana nazo.

Aidha alitoa rai kwa makandarasi kuwa sehemu ya mabadiliko chanya ndani ya sekta ya ukandarasi kwa kuhakikisha wanazingatia ubora na usimamizi mzuri wa miradi wanayoitekeleza hali itakayowafanya kuaminika Zaidi na kutumiwa sana kwenye utekelezaji wa miradi mingi.

“Sisi makandarasi tunayo nafasi hata ambayo hata ikitengenezwa miongozo ya namna gani, kama hakuna utekelezaji, hata wasimamizi watapata changamoto kwenye kusimamia hivyo, suala la ubora wa kazi zetu ni suala la msingi sana sambamba na ubora wa rasilimali” alisema Mungunasi.

Mafunzo haya yamewakutanisha washiriki zaidi ya 100 kutoka mikoa mbali mbali hapa nchini.