Rais Samia ziarani Ethiopia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:55 AM Feb 14 2025
Rais Samia Suluhu
PICHA:MTANDAO
Rais Samia Suluhu

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kuanza ziara ya kikazi katika Jiji la Addis Ababa nchini Ethiopia kuanzia leo hadi 16 2025 kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Kawaida wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais-Ikulu, mkutano huo unatarajia kuchagua Mwenyekiti Mpya wa Umoja wa Afrika kwa mwaka 2025 atakayechukua nafasi ya Mwenyekiti wa sasa . 

Aidha, Mkutano huo pia utachagua viongozi wapya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ikiwemo Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Makamishna sita.

Vilevile, Mkutano utajadili taarifa ya ushiriki wa Umoja wa Afrika kwenye mkutano wa nchi tajiri duniani (G20), utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika na taarifa kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi. 

Mbali na masuala hayo, mkutano utajadili ajenda kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia iliyopendekezwa na  Tanzania.Kabla ya kushiriki Mkutano wa 38, Rais Samia atashiriki Mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika unaofanyika leo.