Katika juhudi za kuimarisha usimamizi wa hospitali na utoaji wa huduma bora kwa wananchi, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita imezindua Bodi ya Ushauri ya Afya. Lengo kuu la bodi hiyo ni kuhakikisha huduma zinaboreshwa na rasilimali zinatumika kwa ufanisi.
Bodi hiyo, iliyoteuliwa na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama mnamo Novemba mwaka jana, imezinduliwa rasmi leo. Itasimamia uendeshaji wa hospitali, kuhakikisha huduma zinatolewa kwa viwango vya juu na kuongeza uwajibikaji.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombat, amesema bodi hiyo itatoa mwongozo wa usimamizi bora wa hospitali na kusaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wagonjwa.
“Kazeni buti na mfanye kazi kwa uaminifu ili kuwahudumia wananchi ipasavyo. Ushirikiano wenu utasaidia kupunguza rufaa zinazotumwa hospitali za Kanda au Taifa,” amesema Gombat.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Mfaume Salum, amesema kuanzishwa kwa Hospitali ya Rufaa ya Geita kumewezesha kupunguza rufaa zilizokuwa zikipelekwa Bugando, hivyo wagonjwa wanapata huduma za kibingwa karibu zaidi.
“Hadi sasa tunao watumishi 450 na tunaboresha huduma kila siku kuhakikisha wagonjwa wanapata matibabu bora kwa haraka, jambo ambalo limepunguza vifo vilivyosababishwa na kuchelewa kupata huduma,” amesema Salum.
Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Dk. Fadhili Kibaya, amesema bodi hiyo imepewa dhamana ya kusimamia hospitali kwa kipindi cha miaka mitatu, akisisitiza kuwa ushirikiano wao utawezesha utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi hiyo, Manase Ndoroma, ameahidi kushirikiana na wataalamu wa hospitali hiyo ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Sisi ni daraja kati ya wananchi na hospitali. Tutahakikisha tunashirikiana na timu ya wataalamu ili huduma ziboreshwe na malengo ya hospitali yafikiwe,” alisema Ndoroma.
Uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Geita ni hatua muhimu katika mkakati wa serikali wa kuboresha huduma za afya nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED