NAIBU Waziri Mkuu, Dk. Dotto Biteko, amesema Tanzania ina umeme wa ziada wa Megawati 740 na kwamba katika serikali ya awamu hii ya sita inakwenda kukamilisha mipango yake ya miaka mingi ya kuuza umeme nje ya nchi.
Dk. Biteko ambaye ni waziri mwenye dhamana ya Nishati, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua maandalizi ya Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), utakaotumika katika mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuanzia Januari 27 na 28 mwaka huu.
Alisema tayari maandalizi kwa ajili ya kuanza kuuza umeme huo yameanza kwa kujenga laini zitakazotumika kusafirisha umeme huo kwenda nchi jirani ikiwamo Zambia.
“Nchi yetu tunao umeme wa ziada, kwa mitambo yetu yote tuliyonayo tukijumlisha, tuna zaidi ya megawati 740 ambayo ipo tu ambayo tungeweza kuitumia kama tungekuwa na mahali pa kupeleka,” alisema Dk. Biteko.
“Lakini hatuwezi kupeleka huo umeme kwa wenzetu kwa sababu hatuna njia za kuwapelekea. Kwa mfano Zambia, wana changamoto ya mgawo wa umeme kwa muda mrefu, kwa sasa tunajenga laini ya kutoka Iringa, Mbeya kwenda Tunduma, baadaye tuunganishe na wenzetu wa Zambia, na tayari tuko kwenye hatua za mwisho majadiliano ya kuwauzia umeme.
“Ile ndoto ya mliyokuwa mkiisikia kwamba tutauza umeme kwa wenzetu, imesemwa kwa miaka mingi, inakwenda kutokea kwenye awamu ya sita ya serikali. Tayari mikakati hiyo ipo, tumeikamilisha, hivi ninavyozungumza tumeshajiunga na wenzetu wa Kenya, Burundi na Rwanda kupitia mradi wa Rusumo, wakihitaji umeme hata jana tutawapatia,” alisema Dk. Biteko.
Kadhalika, alisema mwezi ujao, wakuu wa nchi hizo tatu wanaoshirikiana kwenye mradi wa Rusumo, watauzindua rasmi mradi huo.
Kuhusu mkutano huo wa wakuu wa nchi, Dk. Biteko alisema maandalizi yamekamilika kwa asilimia 95 na kwamba marais wengi pamoja na wakuu wa taasisi za kimataifa wamethibitisha kushiriki.
Alitaja sababu zilizochangia Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo kuwa ni pamoja na kupiga hatua kwenye diplomasia pamoja na kwenye sekta ya nishati hususani kwa kufanikiwa kupeleka umeme vijiji 12,318 na vitongoji 64,274 na tayari vitongoji 34,000 vimekwisha kusambaziwa.
Alisema faida zitakazopatikana kutokana na uwapo wa mkutano huo ni pamoja na kuongezwa kwa kasi ya Watanzania watakaounganishwa na umeme ifikapo mwaka 2030 hadi kufikia milioni 13.5. badala ya milioni 5.2.
Faida nyingine zitakazotokana na mkutano huo ni kuongezeka kwa fursa za uwekezaji, kuimarisha biashara na kuongeza heshima ya Tanzania kimataifa.
Alisema mpaka sasa marais wengi na wakuu wa taasisi za kimataifa wamethibitisha kushiriki katika mkutano huo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema mkoa huo ni mwenyeji wa mkutano huo, wamekubaliana na kikosi cha usalama barabarani kupunguza foleni barabarani na kupunguza baadhi ya usafiri ikiwamo bajaji na pikipiki.
Pia, aliwataka wenye malori ambao yanapaki pembezoni mwa barabara inayotoka uwanja wa ndege kwenda mjini, kuyaondoa haraka ifikapo Januari 20.
“Kila mwenye lori atafute eneo la kuliegesha, kwa sababu zile barabara ni lazima ziwe wazi ili kupendezesha mji wetu,” alisema Chalamila.
Alisema wamejiandaa kunadi huduma mbalimbali ikiwamo za afya, mazoezi, utalii na watakuwa na maonesho ya baadhi ya bidhaa na kwamba wamepata taa 400 ambazo zitafungwa ili kusaidia kufanyika kwa biashara saa 24.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED