Wafanyabiashara wakoshwa maboresho Bandari ya Dar

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:12 AM Jan 16 2025
 Bandari ya Dar.
Picha: Mtandao
Bandari ya Dar.

MABORESHO ya miundombinu katika Bandari ya Dar es Salaam yamepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za kushughulikia mizigo kutoka Dola za Marekani 8,000 hadi Dola 3,000.

Khamis Livembe, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam baada ya kuzuru bandarini huko na wafanyabiashara wenzake na kuona uboreshaji wa miundombinu na utendaji wa bandari hiyo.

Livembe alisisitiza kwamba wawekezaji wawili binafsi wanaoendesha bandari hiyo, wamechangia kwa kiwango kikubwa kuboresha ufanisi wake kiutendaji.

Alisema kuwa muda wa kawaida wa kutoa mizigo kutoka kwenye meli moja umepungua kwa kiasi kikubwa kutoka wastani wa siku 23-24 hadi wastani wa siku tatu pekee.

Kusimikwa kwa mitambo ya kisasa ya kubeba mizigo na mashine zinginezo kumeongeza uwezo wa bandari hiyo katika kushughulikia mizigo.

"Ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam umepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za usafirishaji, hivyo kutoa nafuu kwa watumiaji wa mwisho," alisema Livembe.

Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abeid Ngalusi, alikiri uwekezaji huo umeboresha shughuli za bandari hiyo.

Alisema kuwa muda wa meli kusubiri kuingia bandarini umepunguzwa hadi sifuri (meli inaingia bandarini moja kwa moja badala ya kusubiri), huku muda wa kupakua mizigo ukiwa umepungua kutoka wastani wa siku 10 hadi siku tatu.

Hata hivyo, Ngalusi alibainisha changamoto mpya za wasafirisha mizigo wengi hawaondoi mizigo yao kwa wakati, jambo linalosababisha msongamano.

"Bandari si kituo cha kuhifadhi mizigo," alisisitiza. "Wasafirishaji mizigo lazima wahakikishe wanatoa mizigo yao kwa wakati ili kuachia nafasi kwa mizigo mingine."

Hivi sasa, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inahudumia asilimia 30 ya mizigo ya ndani na asilimia 60 ya mizigo ya kupitisha kwenda nchi jirani kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zambia na Rwanda.

Elitunu Malamia, Meneja Uhusiano wa Kampuni wa DP World, alisisitiza malengo ya kampuni hiyo kwa bandari hiyo ni kuwa ifikapo mwaka 2030, bandari itakuwa na uwezo wa kushughulikia kontena 30,000 kwa siku, likiwa ni ongezeko kubwa kutoka kiwango cha sasa.

Alisema kuwa kwa sasa, bandari inashughulikia meli 16 kwa mwezi na ina mipango ya kushughulikia kontena 220,000 katika siku zijazo.

Mnamo mwaka 2023, TPA ilitia saini mkataba wa makubaliano wa miaka 30 na Kampuni ya DP World kwa ajili ya kuboresha na kusimamia shughuli za bandari hiyo.