KLABU ya Yanga imesema msafara wa wachezaji na viongozi wa MC Alger kutoka Algeria uliotarajiwa kuwasili nchini jana alfajiri haujaonekana, hivyo hali hiyo imewataka kuongeza umakini kuelekea mchezo utakaofanyika keshokutwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, imeelezwa.
Yanga itawakaribisha MC Alger katika mechi ya raundi ya sita ya Kundi A utakaochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo wenyeji wanahitaji ushindi wa aina yoyote ili kufuzu hatua ya robo fainali.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema taarifa kutoka kwa uongozi wa MC Alger zilieleza walitarajia kuwasili nchini jana alfajiri lakini ugeni huo haujaonekana na badala yake walishuhudia ujio wa mashabiki na baadhi ya maofisa wa timu hiyo wakiwasili kwa 'mafungu'.
Kamwe alisema hii yote haifanyiki kwa bahati mbaya, badala yake ni mpango mkakati na unaoratibiwa na wapinzani wao kwa ajili ya kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mchezo huo.
"Taarifa ambazo tunazo wapinzani wetu walipaswa kuingia nchini alfajiri ya kuamkia leo (jana), lakini mpaka sasa hatujawaona na sisi kama klabu tulifanya wajibu wetu lakini hawakutokea, tukipata taarifa rasmi basi tutawajuza. Kimsingi tunahitaji kuwaona uwanjani Jumamosi mengine hayatuhusu," alisema Kamwe.
Aliongeza kwa mabadiliko hayo yanawapa 'picha' kubaini wapinzani wao pia wamedhamiria mapambano ya kusaka ushindi au sare ili wasonge mbele.
"Niwaambie tu wanachama na mashabiki wa Yanga, wanapaswa kuja uwanjani ili kuwasapoti wachezaji kwa sababu mechi haitakuwa rahisi kama ambayo inafikiriwa. Nafikiri mnaona wanavyofanya ujanja ujanja wanakuja kwa mafungu mafungu. Wamedhamiria kuja kupata pointi tatu au moja, hivyo kila Mwana-Yanga anapaswa kujua kuna jukumu zito la kuujaza uwanja," Kamwe alisema.
Aliwapongeza wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kufuatia mauzo ya tiketi kwenda vyema, hivyo anaamini mpaka Jumamosi angalau mashabiki watafikia idadi ya 50,000 au 60,000 ambayo ndio uwezo wa kujaza uwanja.
"Niwapongeze mashabiki na wanachama, tiketi nyingi tayari zimenunuliwa kabla hata mkutano wa hamasa au klabu kutangaza rasmi uuzwaji wa tiketi, mwamko umekuwa mkubwa sana, wananchi wameonyesha kwa vitendo kwa kiasi gani wanaitaka mechi," Kamwe alisifia.
Kuhusu hali ya wachezaji alisema karibu wote wapo katika hali nzuri, isipokuwa Yao Kouassi huku Maxi Nzengeli akiendelea vizuri.
"Mchezaji wetu Yao atakuwa nje kwa kipindi kisichopungua wiki nne na kisichozidi wiki sita. Maxi anaendelea vizuri na maozezi, kama mwalimu ataona utimamu wake wa kimwili unafaa kucheza, basi mchezo ujao atamtumia lakini kimsingi kwa sasa yupo vizuri," aliongeza.
Yanga na MC Alger zote zinawania nafasi moja, baada ya Al Hilal yenye pointi 10 kufuzu, licha ya kutokuwa na uhakika wa kumaliza ikiwa kinara wa kundi hilo.
Yanga, iko nafasi ya tatu ya msimamo ikiwa na pointi saba, ambapo inahitaji ushindi pekee ili kufuzu, ambapo itafikisha pointi 10 na kuiacha MC Alger ikisalia na pointi nane.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED