BAADA ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kutoa adhabu kwa Simba kucheza bila mashabiki katika mechi ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Costantine kutoka Algeria, Kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids, amesema hilo ni pigo kwa Wekundu wa Msimbazi.
Simba itaikaribisha CS Constantine katika mechi ya mwisho ya Kundi A itakayochezwa kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
CAF pia imeipiga Simba faini ya Dola za Marekani 40,000 kufuatia vurugu za mashabiki wake katika mechi dhidi ya CS Sfaxien ambayo ilichezwa hapa nchini na wenyeji kupata ushindi wa mabao 2-1.
CS Sfaxien pia wamepigwa faini ya Dola za Marekani 40,000 kutokana na wachezaji, viongozi na mashabiki wake kufanya vuguru katika mchezo huo, CAF wametoa siku 60 za kulipa faini hiyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Fadlu alisema mashabiki ni muhimu katika mchezo huo wa kusaka nafasi ya kuongoza kundi lao lakini 'hakuna namna' ya kuikwepa adhabu waliyopewa.
Fadlu alisema wamejiandaa kupambana ili kusaka ushindi na hatimaye kumaliza hatua hiyo ya makundi wakiwa kileleni baada ya timu zote mbili tayari zimeshatinga robo fainali ya michuano hiyo.
"Muhimu zaidi kwetu ni kuhakikisha tunashinda na kupata pointi tatu, najua mashabiki ni muhimu sana, lakini ni lazima tupambane ili tushinde hata kama mashabiki wetu hawatakuwepo, huko watakapokuwepo watatuombea.
Jukumu la kwanza la kuingia robo fainali limefanikiwa, sasa hivi tunahitaji ushindi ili kumaliza kwa heshima, linaweza hata kama hatutakuwa na mashabiki wetu, tutapambana kwa dakika zote, tunataka kumaliza katika nafasi ya kwanza kwenye kundi letu," alisema Fadlu.
Kocha huyo alisema wachezaji wake wameonyesha wana na morali na mchezo huo ambao wanataka kulipiza kisasi cha kufungwa katika mchezo wa kwanza waliocheza ugenini ambao walipoteza kwa mabao 2-1.
"Mchezo huu kila mchezaji ana ari na morali kubwa, tunataka kwanza kulipiza kisasi cha kufungwa mchezo wa kwanza, lakini lengo kuu kupata pointi tatu tuweze kuongoza kundi letu," Fadlu alisema.
Nahodha wa Simba, Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr', alisema wanaendelea na maandalizi yao huku wakifuata kile wanachoambiwa na kocha wao kuelekea katika mchezo huo.
"Sisi tupo vizuri, tunaendelea na maandalizi yetu, kila mchezaji yupo vizuri na yupo tayari kwa mchezo huu, tunaamini tutawapa furaha mashabiki wetu ambao hawatakuwepo uwanjani," alisema beki huyo.
Wakati huo huo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, kikosi chao kiliingia kambini jana kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo.
Ahmed alisema wataingia katika mechi hiyo kwa lengo moja la kusaka pointi tatu ili kuwarahisishia kuanzia ugenini kwenye hatua ya robo fainali.
"Tukimaliza wa kwanza, robo fainali tutaanzia ugenini, tutamalizia nyumbani, tutakuwa na nafasi nzuri ya kuingia nusu fainali. Kwenye kundi tumezifunga timu mbili na alikuwa bado huyu wa Jumapili, hivyo na yeye anatakiwa apate pumzi ya moto.
Wapinzani wetu CS Constantine wako njiani kuja Tanzania na maofisa wetu wa Simba wako uwanja wa ndege kuwapokea," Ahmed alisema.
Ushindi wowote katika mchezo huo utaifanya Simba kumaliza katika nafasi ya kwanza kwenye kundi lao huku sare ya aina yoyote itawapa uongozi CS Constantine.
Timu hizo zote zimefuzu hatua ya robo fainali, CS Constantine ikiwa na pointi 12 ikifuatiwa Simba yenye pointi 10, Bravos do Maquiz ya Angola iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba wakati CS Sfaxien ya Tunisia wanaburuza mkia baada ya kufungwa michezo yote mitano.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED