ACT-Wazalendo imetangaza kuanza kwa mchakato wa ndani ya chama wa wanachama kujitokeza na kutangaza nia ya kugombea nafasi mbalimbali za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kuanzia jana.
Hatua hiyo ni utekelezaji agizo la Halmashauri Kuu ya Chama Taifa iliyoelekeza chama kuweka utaratibu wa wanachama kutangaza nia ya kugombea nafasi za udiwani, udiwani wa viti maalumu, ubunge, ubunge wa viti maalumu na urais.
Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alitangaza kuanza kwa mchakato huo jana alipokutana na waandishi wa vyombo vya habari kwenye ofisi za Makao Makuu ya chama mkoani Dar es Salaam.
Alitaja mambo ya kuzingatiwa kwenye mchakato huo ni pamoja na watiania kutakiwa kujisajili kwenye orodha ya watiania kwa ngazi husika kwa kujaza fomu maalumu.
"Watiania wa udiwani na udiwani wa viti maalumu watajaza fomu ngazi ya kata, ubunge na ubunge wa viti maalumu ngazi ya jimbo na watiania wa urais watajaza fomu maalumu Ofisi ya Makao Makuu ya chama," alifafanua.
Ado alisema watiania wanaruhusiwa kujitangaza kupitia njia mbalimbali ikiwamo kuzungumza na waandishi wa habari. Idara ya Habari, Uenezi na Uhusiano na Umma Ngazi ya Taifa kwa kushirikiana na viongozi wa mikoa na majimbo imeagizwa kuhakikisha kuwa watiania wote wanapata nafasi ya kujitangaza kupitia kurasa za mitandao ya kijamii ya chama na kuwaunganisha na waandishi wa habari na kusambaza taarifa za watiania hao.
Katibu Mkuu Ado alisema viongozi wa mikoa, majimbo na kata wameagizwa kuwaruhusu watiania kutumia ofisi za kata, majimbo na mikoa kutangaza nia zao. Kwa ngazi ya urais wa Tanzania, watiania wanaruhusiwa pia kutangaza nia kupitia Ofisi ya Makao Makuu ya chama.
"Watiania wanapaswa kujipima kwa kuzingatia vigezo vya watiania ambavyo vimewekwa na Halmashauri Kuu ya Chama. Vigezo hivyo ni pamoja na kutimiza sifa za kugombea nafasi husika zilizoainishwa na sheria za nchi na Katiba ya ACT Wazalendo Toleo la Mwaka 2024 pamoja na Kanuni za Uchaguzi za Chama.
"Sifa nyingine ni kuwa na haiba, maadili, uwezo wa kujieleza na maono yanayoendana na nafasi ambayo mtiania anakusudia kugombea. Watiania watapimwa pia kwa ushiriki wao katika ujenzi wa chama.
"Viongozi wa ngazi husika wameagizwa kuweka utaratibu wa kuwashirikisha watiania katika shughuli za ujenzi wa chama katika ngazi husika na kutunza taarifa za ushiriki wao," alisema.
Katibu Mkuu Ado alisema chama kitaweka utaratibu wa usaili kwa watiania kabla ya taratibu za kikatiba za uteuzi wa wagombea. Taratibu na jopo la usaili vitatangazwa baadaye kwa ngazi za ubunge na urais.
Alisema usaili huo utakuwa wazi kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari, akisisitiza kuwa wanachama wote wa ACT Wazalendo wenye sifa za kugombea udiwani, udiwani wa viti maalumu, ubunge, ubunge wa viti maalumu na urais wanakaribishwa kutangaza nia kwa utaratibu ambao umeelekezwa.
Katibu Mkuu huyo pia alisisitiza Chama cha ACT-Wazalendo kitaendeleza utamaduni wake wa kuendesha michakato ya uchaguzi kwa kuzingatia misingi ya uwazi, demokrasia na usawa.
TUME HURU
Alipoulizwa sababu za ACT kuamua kushiriki Uchaguzi Mkuu mwaka huu licha ya kuwapo madai ya kutokuwapo uhuru kwa wasimamizi wa uchaguzi huo, Ado alisema:
"Sisi (ACT-Wazalendo) pia hatukubaliani kabisa na tume ya sasa kwa sababu hatujaridhika na kile kilichofanyika kuifanya iwe huru. Na ndiyo maana uongozi wa chama umeshatoa kauli kuhusu hili, hata kutotambua matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopita.
"Tutapaza sauti yetu kwa kushirikiana na wadau wengine wa demokrasia kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unasimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi.
"Michakato ya ndani inaendelea kuhakikisha tunajiandaa kwa uchaguzi huo. Kama huandai wagombea, hata kama kukiwa na Tume Huru ya Uchaguzi, huwezi kufanya vizuri katika uchaguzi huo. Ndiyo maana tunajiandaa."
Kuhusu yanayoendelea katika uchaguzi wa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kama wako tayari kuwapokea watakaoshindwa kwenye uchaguzi huo na kuwapa nafasi ya kuwania uongozi serikalini, Ado alisema.
"Waandishi mnatumika sana, na inaonekena hili mmekubaliana hamtaliacha. Majibu yangu ni yaleyale, na leo (jana) pia ni yaleyale -- ACT Wazalendo ni chama makini cha siasa, kina mipango yake, kina mikakati yake. Ndiyo inayokifanya kuwa chama kinachokua kwa kasi zaidi nchini. Hata hao CHADEMA wanalitambua hili.
"Kitakuwa chama cha ajabu sana kikaacha mipango yake, kikaacha mambo yake na kuzungumzia yanayoendelea CHADEMA. Kwenye hili 'no comments'. Tunawatakia heri CHADEMA wafanye uchaguzi wao, wamalize salama.
"Wakitokea watu wakataka kujiunga na ACT, tunawakaribisha na tutawapokea kwa mikono miwili. Mtaji wa chama cha siasa ni watu. ACT tuko tayari kuwapokea wapiganaji wote waliokataa tamaa au wamefadhaishwa na vyama vyao.
"Ukichoshwa na CCM, CUF njoo ACT Wazalendo. Huku ndiko kimbilio la wasioridhishwa na vyama vyao. Ndiyo maana hata Maalim Seif Sharif Hamad alipoona amechoshwa na CUF, alichagua ACT.
"Kuhusu kuwapa nafasi ya kugombea, tunao wanachama wenye sifa za kugombea nafasi zote. Tunao utaratibu wa usaili wa wagombea na Mkutano Mkuu huamua nani apeperushe bendera ya chama.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED