Wakulima kupewa miche milioni 20 ya kahawa

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 08:59 AM Jan 16 2025
Miche ya kahawa.
Picha:Mtandao
Miche ya kahawa.

SERIKALI imeanza kusambaza miche milioni 20 ya kahawa na kugawa bure kwa wakulima wa mikoa inayostawisha zao hilo ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo nchini.

Mpango huo umetangazwa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa  kuhusu maandalizi ya mkutano wa tatu wa nchi zinazozalisha kahawa Afrika (G25) utakaofanyika nchini mwezi ujao jijini Dar es Salaam. 

Bashe, alisema miche hiyo itazalishwa katika vituo vya kahawa vilivyopo  nchini na kugawa kwa wakulima ili kufikia lengo la serikali kulifanya kuwa ni miongoni mazao ya kimkakati yanayolimwa nchini. 

"Serikali imeanza kusambaza miche milioni 20 kwa wakulima wadogo wa zao hilo katika maeneo mbalimbali na hii ni kuhakikisha wakulima wote wanapiga hatua kupitia kilimo hicho," alisema Bashe. 

Alisema kahawa ni moja ya kilimo ambacho kinaweza kuwasaidia vijana kujiajiri kupitia biashara ya kinywaji hicho katika maeneo tofauti. 

Akizungumzia kuhusu maandalizi ya mkutano huo wa siku mbili utakaofunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kaulimbiu yake ni “Kufungua Fursa za Ajira kwa Vijana Kupitia Uboreshaji wa Sekta ya  Kahawa Afrika. 

 Bashe, alisema mkutano huo ni matokeo ya azimio lililopitishwa katika  Mkutano wa 61  uliofanyika Novemba 18 mwaka 2021  Kigali nchini Rwanda. 

Alifafanua kuwa lengo ni kufanya tathmini ya mapungufu na changamoto zinazosababisha kuzorota kwa Sekta ya Kahawa  Afrika. 

Baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, mkutano wa kwanza wa nchi hizo ulifanyika Kenya Mei mwaka 2022 na kupitisha Tamko la Nairobi.

Tamko hilo liliweka mkakati wa kuingiza kahawa kama bidhaa  muhimu ya kimkakati katika Umoja wa Afrika (AU)  na agenda mwaka 2063 ya AU. 

Mkutano wa pili ulifanyika Kampala nchini Uganda, Agosti mwaka 2023 na  kupitisha Tamko la Kampala  kuwaomba wakuu wa nchi hizo kuunga mkono kuidhinishwa na 

kujumuishwa kahawa bidhaa muhimu ya mkakati katika ajenda hiyo ya mwaka 2063 ya AU.