Lema: Sitagombea ubunge Mbowe akishinda CHADEMA

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 10:09 AM Jan 15 2025
Godbless Lema.
Picha:Mtandao
Godbless Lema.

BAADA ya ukimya wa muda mrefu, hatimaye Godbless Lema, amechagua upande wa kuunga mkono katika kinyang`anyiro cha nafasi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Mwenyekiti huyo mstaafu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini ametangaza rasmi atamuunga mkono Tundu Lissu katika kinyang`anyiro hicho, huku akiwa na lingine la ziada kwamba hatogombea ubunge jimboni Arusha Mjini ikiwa Freeman Mbowe atachaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa chama hicho.

Lema alitangaza hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam.

Desemba 24 mwaka jana, Nipashe ilizungumza na Lema kutaka kujua upande anaounga mkono kati ya vigogo hao wawili wanaogombania nafasi ya uenyekiti wa chama, lakini alisema amejifungia kufanya maombi ili Mungu amwongoze kujua upande upi aunge mkono, akiahidi angetangaza baadaye.

Katika mkutano na waandishi jana, Lema alimshauri Mbowe ajitoe kwenye kinyang'anyiro hicho na kumwachia Lissu huku akimsisitiza asikilize ushauri wa familia yake iliyomwomba apumzike.

Lema alisema anaamini familia ya Mbowe iliongozwa na Mungu kumwambia apumzike na akatoa tahadhari kwamba kuna hatari kubwa mwenyekiti huyo wa sasa wa chama hicho akapoteza heshima yake endapo atang`ang`ania kugombea nafasi hiyo.

"Mimi ushauri wangu kwa mwenyekiti, sikiliza familia yako, imeongozwa na Mwenyezi Mungu kukwambia upumzike. Akipumzika atakuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya chama wa kudumu mpaka siku atakapofariki dunia, maana yake anaendelea kutoa msaada, mawazo," alisema Lema.

"Hiki chama ni mtoto wake, amekuwa nacho, hataacha kianguke, atakuwa kwenye Kamati Kuu ambayo ndiyo inafanya kazi kubwa kwa niaba ya Mkutano Mkuu na Baraza Kuu. Lissu akishindwa itaitishwa kamati itamwondoa," aliongeza.

Lema alisema ni vyema chama kufia kwenye mikono ya mtu mwingine kuliko chama kifie kwa Mbowe.

"Yaani mimi ningekuwa Mwenyekiti (Mbowe), ili kulinda heshima yangu ya miaka 30, kuliko chama kifie kwangu mimi ambaye nimejenga 'legacy' kubwa, nitaruhusu hicho chama kifie kwa mtu mwingine," alisema Lema.

Aliwashangaa wale ambao wanasema bila Mbowe, CHADEMA itakufa, akihoji "Hivi Mwenyekiti (Mbowe) akifa au anaumwa, akashindwa kufanya kazi, chama kitakufa?"

Lema pia alimshauri Mbowe kusikiliza na kuzingatia maoni wa wananchi wanayotoa kupitia mitandao ya kijamii kuhusu nafasi hiyo anayogombania tena.

"Tukipuuza hayo maoni, uchaguzi tukakwenda keshokutwa pale, akashindwa, legacy yake itakufa siku hiyo hiyo. Kutakuwa na shangwe ya kumwangusha mwasisi na mimi ninaona hii ni hatari kwa ndugu yangu," alisisitiza.

Lema alisema anaamini kwamba atakuwa kwenye wakati mgumu kwa kuchagua kuwa upande wa Lissu na kwamba anaamini alichochagua ni demokrasia na si utamaduni.

Lema alisema yupo kiongozi mmoja ndani ya chama hicho ambaye alikwenda mpaka kwa mama yake kumwomba amshauri kuhusu msimamo wake huo.

"Mama yangu anaweza asinielewe, baba yangu anaweza asinielewe. Na kuna mtu mmoja amekwenda hadi kijijini kule akamwambia mama kwamba 'mwambie Lema asimwache kaka yake, maana akishinda, Lema atakuwa kwenye wakati mgumu, anaweza hata akapoteza ile nafasi yake ya kugombania ubunge'," alidai Lema.

Lema alisema hafanyi kazi ya siasa ili kuwa kiongozi bali kwa sababu ana wito wa kufanya kazi hiyo kwa ajili ya wajukuu wa nchi hii waje wawe na maisha mazuri.

"Haya maisha ni mafupi sana, yaani pilika zote hizi... ninakwenda jela, ninakimbiza familia, ili tu eti nije kuwa mbunge! Hebu jamani tusidhalilishane, sitagombania ubunge Arusha Mjini mwaka 2025 halafu nitaendelea kuwa mwanaharakati huru.

"Kwa hiyo nitamuunga mkono Lissu na Mwenyekiti (Mbowe) akishinda sitagombania ubunge Arusha Mjini," alisisitiza Lema.

Alisema atakuwa tayari kumuunga mkono na kumsaidia kumpigia kampeni atakayegombea kwenye jimbo hilo kupitia chama chao hicho, hata kutumia rasilimali zake.

Lema pia alisema: "Hata yakiitishwa maandamano ya kudai Katiba Mpya na tume huru nitakuwa mbele, na nikigundua kuwa mimi kuwa mwanachama wa chama hiki ni kero kwao, nitakuwa mwanaharakati huru, lakini kamwe sitafanya kazi ya CCM (Chama Cha Mapinduzi)."

Lema pia alisema atakuwa tayari kurudi tena kwenye vyombo vya habari kupambana na wapambe wa Mbowe endapo watatoka hadharani na kuanza kumshambulia baada ya kuweka msimamo wake huo.

"Mbowe ni kaka yangu, tunafahamiana, ananijua na mimi ninamjua vizuri sana, niwaonye wapambe msinifanye niitishe mkutano mwingine na waandishi wa habari, chukulieni kama hili ni tendo langu la kidemokrasia na mimi huwa ninaongozwa na Mungu. Msinitukane, msinidhalilishe kwa sababu ninamuunga mkono Lissu. 

"Mkifanya hivyo mimi ninaweza kuamua kuja kujibu, tutagombana na ndugu yangu... nisaidieni mimi na ndugu yangu tukikutana Machame Krismasi tushikane mkono," alisema Lema.

Lema alisema anaamini kwa msimamo wake huo, hata familia yake haitafurahia.

Aliwaomba wajumbe kutoka Kanda zote kumpigia kura Lissu na kuepuka kushawishiwa kwa namna yoyote.

“Wajumbe ni hatari sana, ninataka niwaambie hivi, ukiona kuna mtu anataka kununua uongozi ambao hana mshahara, huwa kuna mahali analipwa mshahara kwa ajili ya huo uongozi na wajumbe mkikubali kupewa pesa, mkapiga kura kwa ushawishi wa pesa, jambo la msingi ni sahihi CCM kuendelea kutawala nchi hii?

"Kama wajumbe wa CHADEMA, wanaweza kupiga kura ya nguvu ya pesa na siyo utashi na uelewa, tuna tatizo kubwa kama nchi. Chama cha siasa cha upinzani mnatakiwa kuwa na aina ya viongozi ambao akiona bunduki anaifuata anasema moyoni hata nikifa, ninakufa kwa sababu ninapigania kweli," alisema Lema.

Lema pia alitumia mkutano huo kutangaza kumuunga mkono John Heche katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti anayogombea, akisisitiza kuwa:

"Mimi ningekuwa na mamlaka ya kichama, Wenje (Ezekiel - anayechuana na Heche), hakutakiwa kuwa mwanachama wa CHADEMA leo."

Lema pia alisema kuwa Lissu akishinda, watamwomba msamaha Dk. Wilbroad Slaa na watamrejesha kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.

"Ushauri wangu kwa kaka yangu Freeman Mbowe, msaidie Lissu kuwa mwenyekiti, kama una shaka na uongozi wake, utakuwa mjumbe wa Kamati Kuu, sina kinyongo na wewe kaka yangu... tukikutana Machame tusalimiane lakini ikiwa itashindikana kusalimiama kwa sababu ya msimamo huu mimi sitajali sana, nitaendelea na maisha yangu kama kawaida," alisema.

Lema alidai kukataa kwake kugombea tena nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini ni baada ya kugundua kulikuwa na mpango uliosukwa ili kuwaondoa katika mfumo wa uongozi ndani ya chama hicho.

Alidai walengwa wakuu katika mpango huo ni yeye, Heche, Peter Msigwa na Lissu.