UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa X inayomkabili mwanasiasa mkongwe, Dk. Wilbroad Slaa umedai haujui aliko mshtakiwa huyo na pia haujui sababu za kutokupelekwa mahakamani.
Jopo la mawakili watano wanaomtetea Dk. Slaa, akiwamo Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwambukusi, limedai kushangazwa na Jamhuri kutokujua aliko mshtakiwa wakati wao walizuia dhamana yake kwa madai ya kulinda usalama wake.
Kesi hiyo iliendelea kwa mabishano mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuanzia saa 5:12 asubuhi hadi saa 6:22 mchana bila mshtakiwa kuwapo, hoja mbalimbali ziliibuliwa ikiwamo uhalali wa mashtaka.
Kutokana na mabishano hayo makali ambayo yalikuwa hayana mwafaka kwa pande zote mbili, Hakimu Nyaki alifikia uamuzi wa kuwaita mbele mawakili wote 11 ili wazungumze kwa utaratibu wa kuelewana kwa pande zote.
Hata hivyo, mawakili hao waliporudi kwenye viti vyao, minong'ono ya chini ikiendelea na walipopewa nafasi ya kuzungumza mabishano yaliendelea ya kusikilizwa kwa kesi hiyo bila mshtakiwa kuwapo, utetezi wakitaka iendelee ilhali Jamhuri wakipinga hilo.
Mbali na Mwambukusi, mawakili wengine ni Peter Madeleka, Hekima Mwasipu, Sanga Melikiole na Sisty Aloyce ambao wote wanamwakilisha Dk. Slaa huku wakidai afya yake si nzuri kukaa mahabusu, anatakiwa awe chini ya uangalizi wa familia yake.
Jopo la Mawakili wa Serikali linaongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Tawabu Issa, Clemence Kato, Michael Ngoboko, Nura Manja, wakisaidiana na Mawakili wa Serikali Abdon Bundala na John Mwakifuna, walipinga kesi kuendelea kusikilizwa kutokana na maombi yalikuwa mahakamani.
Baada ya utambulisho wa mawakili wa pande zote, Hakimu Nyaki aliuliza alikokuwa mshtakiwa. Wakili Issa alidai kwamba wao kesi ilipoitwa walijua yupo na hawakupata sababu za kutofikishwa mahakamani.
"Ninyi ndio mmemleta mahakamani, ndio mmezuia dhamana yake kwa sababu ya usalama wake na amri ya mahakama leo alitakiwa awapo mahakamani, lakini cha kushangaza na wao wanashangaa kutokuwapo kwake, huo usalama wanaosema uko sehemu gani?
"Wenye wajibu wa kumleta ni wao, hatujaja hapa kuleta utani, tunaomba wawajibike kwa hili," alidai Wakili Madeleka.
Hakimu Nyaki akahoji 'hatuwezi kuendelea bila yeye kuwapo (Dk. Slaa)?. Wakili Mwabukusi akadai "tunaomba tuendelee bila yeye kuwapo. Mahakama iweze kutoa uamuzi kwa sababu ina uwezo wa kusikiliza jambo hili bila kuwapo mtuhumiwa."
Akijibu hoja hiyo, Wakili Issa alidai wamesikia mawasilisho ya kuendelea na kesi hiyo bila mshtakiwa kuwapo, lakini kumbukumbu za mahakama zinaonesha kuna pingamizi la dhamana.
"Yaliyowasilishwa ni mambo kwa kuwa tuliyawasilisha kwa hati ya faragha na kiapo tulitegemea kupata kiapo kinzani kutoka kwa mjibu maombi Dk. Slaa kisha tupangiwe tarehe nyingine ya kusikilizwa," alidai Wakili Issa.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Madeleka alidai hoja ya kuendelea au la tayari Mwambukusi ameomba kuendelea bila Dk. Slaa kuwapo kwa sababu hakuna sheria inayokataza hilo.
"Tupo tayari kusikiliza maombi ya dhamana na pia tupo tayari kusikiliza maombi madogo yaliyofunguliwa," alidai.
Baada ya Hakimu Nyaki kusema kwamba kesi itasikilizwa kwa siku tatu mfululizo, Wakili Mwambukusi alidai Dk. Slaa amekamatwa na kushtakiwa kinyume cha sheria, anaomba isikilizwe hata usiku kutokana na afya yake kwa sababu hajapatikana na hatia.
"Mheshimiwa, kesi hii tunayozungumzia mshtakiwa yupo mahabusu, si uraiani, tunaomba tusikilizwe kwa njia ya mdomo na si kwa maandishi kwa sababu ya muda," alidai.
Hata hivyo, upande wa Jamhuri ulidai kuwa hauwezi kuendelea na usikilizwaji huo wa maombi ya dhamana, ambapo Wakili Madeleka akidai wanaweza kuendelea. Wanaomba isikilizwe Jumatano ya wiki hii.
"Hatuna shida ya juu ya usikilizwaji lakini na sisi tuna mapendekezo yetu ni tarehe ya usikilizwaji angalau iwe Ijumaa kwa sababu mawakili wengi hapa watakuwa kwenye kesi zingine za uhujumu uchumi," alidai Issa.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Januari 17, 2025 saa tatu asubuhi kwa ajili ya kusikilizwa.
Hata hivyo, Wakili Madeleka aliwasilisha pingamizi la kutokuwa na uhalali wa hati ya mashtaka kwa sababu sheria inaeleza kwamba upelelezi ukikamilika ndipo mshtakiwa apelekwe mahakamani, lakini Dk. Slaa alifikishwa mahakamani bila upelelezi kukamilika.
Ilidaiwa kuwa Dk. Slaa alitenda kosa hilo Januari 9, mwaka huu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mtandao huo wa kijamii, akitumia jukwaa lililosajiliwa kwa jina la Maria Salungi Tsehai @MariaSTsehai kwa lengo la kupotosha umma.
Ilidaiwa kuwa kupitia jukwaa hilo, Dk. Slaa alichapisha ujumbe uliosomeka "wakubwa wametafutana, nikisema wakubwa ninamaanisha Mwamba na Samia, na wala hatuna maneno ya kumung'unya... na kimsingi wamekubaliana, Suluhu Samia amekubali atatoa pesa, Suluhu Samia amekubali ataongeza nguvu ya pesa, ni dhahiri atatoa pesa... hizo ni hela za watanzania wanazichezea Samia na watu wake.
"Samia toka muda mrefu haangaikii tena maendeleo ya nchi, anahangaikia namna ya kurudi Ikulu, na namna yake ya kurudi Ikulu ni kwa njia hizo kama kumsaidia mtu kama Mbowe."
Upande wa Jamhuri ulipinga ombi hilo la upande wa utetezi ukidai umewasilisha kiapo kupitia mfumo wa mahakama kupinga dhamana ya mshtakiwa huyo kilichoapwa na SSP George Bagyemu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED