Ninapoondoka Tanzania, napenda kumshukuru kila Mtanzania kwa kunikaribisha mimi na mke wangu Linda katika nchi yenu nzuri.
Toka tulipowasili humu nchini mwezi Januari 2023, kumekuwa na matukio mengi ya kuvutia katika kipindi hiki cha miaka miwili iliyopita.
Mwanzoni kabisa mwa kipindi changu cha kuhudumu humu nchini, Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris alitembelea nchini na kuwezesha kusainiwa kwa Mkataba wa Majadiliano ya Kibiashara kati ya Marekani na Tanzania, unaounganisha sekta za umma na binafsi za Marekani na Tanzania ili kuongeza biashara na uwekezaji wa pande mbili. Ni mwezi uliopita tu, Rais Biden alisafiri kwenda Angola, ambako alikutana na Makamu wa Rais Mpango pamoja na viongozi wengine wa nchi za ukanda huu, kujadili uanzishaji wa Reli itakayokatisha Bara la Afrika (Trans – Africa Continental Railroad). Marekani ni mwekezaji mkubwa katika mradi huu, ambao utanufaisha ukanda mzima kupitia biashara iliyounganishwa zaidi.
Nikitambua kuwa uchumi imara na demokrasia imara huenda sambamba, nilijivunia sana kuwasilisha msaada wa ziada ili kuimarisha maendeleo ya mifumo ya afya, elimu, utawala wa kidemokrasia, na ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Nilipata heshima kubwa ya kukutana na walengwa wa miradi na programu mbalimbali zinazofadhiliwa na Marekani katika safari zangu nyingi nchini kote Tanzania – mazungumzo yangu na watu wa Tanzania ni kumbukumbu nitakayoithamini sana maishani mwangu.
Mara nyingi mimi husema kwamba rasilimali kubwa zaidi ya Tanzania si dhahabu yake, wala si madini yake ya Tanzanite, au hata utajiri wake mkubwa wa wanyamapori na uzuri wake wa asili. Badala yake, rasilimali kubwa na muhimu zaidi ya Tanzania ni watu wake.
Kwa kiwango kikubwa sana, nyakati nilizotumia kukaa na kuzungumza na vijana wa Tanzania wenye maono na hamasa, ndizo zimekuwa nyakati bora zaidi katika kipindi changu cha utumishi kama kama Balozi. Mnamo Agosti 2023, niliungana na viongozi wa vijana kutoka kote nchini walioshiriki katika Mijadala ya Demokrasia kwa Vijana. Tukio hili lililoandaliwa kwa ufadhili wa ubalozi wa Marekani lilibainisha mahitaji ya vijana wa Tanzania na kuwahimiza kushiriki zaidi katika kuimarisha demokrasia ya Tanzania.
Kwa kuwekeza katika akili na fikra changamfu za vijana wa Kitanzania na kuwapa zana na uwezo wa kufanikiwa, tunawekeza katika mustakabali wa Tanzania wenye mafanikio. Ndiyo maana tunahakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata fursa ya elimu yenye ubora wa juu katika vyuo vikuu vya Marekani.
Ndiyo maana tulileta Shindano la Teknolojia la Marekani na Tanzania (U.S.-Tanzania Tech Challenge) nchini Tanzania, tukiwekeza katika mawazo mazuri ambayo wabunifu wa teknolojia wa Tanzania tayari wameyabuni. Zaidi ya wabunifu 100 wa teknolojia walituma mapendekezo ya kuendeleza ushiriki kamilifu wa kiraia kwa Watanzania kwa kutumia zana za kiteknolojia.
Ndiyo maana tulitetea kurejesha mradi wa awali wa Changamoto za Milenia (Millennium Challenge Corporation - MCC) nchini Tanzania, ili kusaidia mustakabali wa kidemokrasia kwa Watanzania wote. Hiyo pia ndiyo sababu niliendelea kutoa kauli za wazi hadharani na kwa faragha kwa ajili ya kuendeleza demokrasia ya Tanzania. Hayo niliyafanya kwa sababu utawala wa kidemokrasia wa Tanzania hautaifanya Tanzania kuwa huru na yenye usawa tu, bali pia utaifanya nchi hii kuwa tajiri zaidi na yenye uwezo wa kutumia kikamilifu zaidi rasilimali yake muhimu zaidi – watu wake.
Ndiyo maana Marekani ni mshirika mkubwa zaidi wa maendeleo wa Tanzania. Na tutaendelea kuwekeza katika kuimarisha sekta ya afya, kupunguza vifo, na kuinua ubora wa maisha ya mamilioni ya Watanzania. Kupitia PEPFAR, tunaunga mkono na kuwasaidia wale wanaoishi na VVU/UKIMWI kuishi maisha yenye afya na ustawi, huku tukidhibiti maambukizi, faida ya kiafya ambayo vizazi vijavyo vya Watanzania vitaendelea kunufaika nayo.
Nimetembelea pembe zote za nchi hii na kukutana na watu wa hali na makundi ya aina mbalimbali. Nimevutiwa na kustaajabishwa sana na jinsi Watanzania wanavyojitoa kwa dhati kuishi katika misingi ya umoja, utu, na ushirikiano.
Tanzania iliyo na umoja, inayozingatia kwa dhati heshima na utu wa kila raia, ni Tanzania itakayoathiri dunia kwa njia chanya. Hiyo ilikuwa ndoto ya Mwalimu Nyerere, na ni ndoto nitakayoitunza moyoni mwangu hata baada ya kuondoka Tanzania.
Daima nitauenzi muda wangu hapa Tanzania. Na nitayaweka moyoni mwangu, katika maisha yangu yote, mafunzo mengi niliyopata kutoka kwa watu wa Tanzania.
Imekuwa heshima kubwa sana maishani mwangu kuhudumu kama Balozi wa Marekani nchini Tanzania.
Imeandikwa Na Balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Michael A. Battle Sr.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED