MATUMIZI ya baruti nchini yameongezeka kutoka wastani wa tani 3,000 kwa mwaka katika miaka ya 1990 hadi kufikia tani 26,516.07 kwa mwaka jana, imeelezwa.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Ramadhani Lwamo, aliyasema hayo juzi jijini hapa wakati akifungua kikao cha kuwajengea uwezo wakaguzi wa migodi na baruti nchini.
Lwamo alisema kuongezeka kwa matumizi hayo kunachangiwa na uchimbaji madini, utafiti wa mafuta, gesi asilia na ujenzi wa miundombinu nchini.
Alisema kuongezeka kwa matumizi hayo kumesaidia kupaa kwa biashara ya baruti nchini tofauti na miaka ya nyuma.
“Matumizi makubwa ya baruti maana yake uchimbaji umeongezeka, hivyo bila udhibiti italeta madhara. Kikao hiki ni kujengeana uwezo lengo kuhakikisha wachimbaji hawapotezi maisha au viungo kwa ajili ya matumizi ya baruti.
“Udhibiti madhubuti ni muhimu, mkadhibiti katika maeneo yenu, itakuwa ni aibu mkaguzi mgodi na baruti eneo lake mtu akapata madhara,” alisema.
Lwamo alisema hadi sasa kuna zaidi ya bohari (magazine) 231, stoo 493, masanduku ya kuhifadhia baruti 279 yaliyosajiliwa kwa ajili ya matumizi migodini na maeneo ya biashara.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi Migodi na Mazingira nchini, Hamisi Kamando, alisema kumekuwa na matukio ya ajali yanayotokana na kukiuka Sheria ya Baruti ya Mwaka 1963, Kanuni za Baruti za Mwaka 1964 na taratibu zingine za usimamizi wa baruti.
Mwanasheria Damian Kaseko aliwataka wakaguzi migodi na baruti kusimamia sheria, kanuni na sera ili kuepusha migogoro na kuwa na mipaka katika utekelezaji wa shughuli zao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED