ZAIDI ya watu 500 wanadai mafao baada ya serikali kufunga maisha ya maua wilayani hapa Mkoa wa Arusha walikokuwa wakifanya kazi miaka michache iliyopita na kupoteza ajira.
Hatua hiyo imekuja baada ya kile walichodai ni jitihada zao za kudai kulipa madai yao kugonga mwamba baada ya mashamba hayo saba ya maua kufungwa mwaka 2020 kutokana na changamoto za uendeshaji, athari za janga la UVIKO-19 na mazingira magumu ya biashara na uwekezaji.
Licha ya watu hao kulilia stahiki zao baada ya kupoteza ajira na wamiliki mitaji, serikali nayo imepata hasara kubwa kwa kupoteza mabilioni ya shilingi kutokana na kukosa kodi ya maua.
Kutokana na madai hayo, baadhi yao, akiwamo Zephania Molell, aliyekuwa mfanyakazi wa Shamba la Maua la Kili Flora Limited (Nduruma Farm), kwa nyakati tofauti jana waliiangukia Wizara ya Kilimo, iwasaidie walipwe stahiki zao, kujikimu kimaisha na kukabiliana na changamoto za kiuchumi zinazowakabili kwa sasa.
“Maisha yetu kwa sasa ni magumu na tuko njiapanda. Tumekusanyika hapa kuiomba serikali itusaidie kulipwa mafao yetu na malimbikizo ya madeni zaidi shilingi bilioni mbili,” alisema Mollel.
Wakati, Theresa Simon, aliyekuwa mfanyakazi wa Shamba la Maua la Mount Meru Flowers, alidai baadhi ya mashamba yalifungwa kutokana na sheria, utitiri wa kodi, tozo na ushuru.
Mwenyekiti wa Wafanyakazi wa Mashamba ya Kili Flora Limited na Mount Meru Flowers, Hamza Sulemani, alisema mpaka sasa hawajapata mafanikio yoyote.
Mashamba mengine yaliyofungwa ni Tengeru Flowers, Tanzania Flowers, Shamba la Arusha Blooms.
Baada ya kuibuka madai hayo, Nipashe ilimtafuta Mwenyekiti wa Halmashauri ya Meru, Jeremiah Kishili na kuthibitisha kutambua suala hilo.
Kishili, aliwataka viongozi wa wafanyakazi hao kufikia ofisini kwake kupata ufafanuzi wa malalamiko yao.
Mwaka 2022, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, aliagiza serikali mkoani Arusha kuanza kufufua mashamba hayo na ikiwezekana kugawanya kwa vijana ili kujiuaji kwa kilimo wakati mchakato mwingine ukiendelea.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED