Wakulima wanawake wa mpunga wajikongoja

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 05:41 PM Jan 15 2025
Mpunga.
Picha:Mtandao
Mpunga.

WAKULIMA wanawake wa mpunga katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wamesema gharama kubwa za zana za kilimo ni kikwazo kwao kujiendesha kibiashara na kuzidi kudidimia kiuchumi kwa kupata hasara.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mmoja wa wakulima hao kutoka Kata ya Mondo, Neema Maziku, alisema wanalazimika kuendesha kilimo cha kawaida kwenye eneo dogo licha ya kuwa na maeneo makubwa na kupata mavuno ‘kiduchu’. 

Neema, aliwaomba wadau wa kilimo kushusha gharama za pembejeo ili kukidhi mahitaji kama njia ya kuwasaidia kuachana na kilimo cha kutumia jembe la mkono kwenye mashamba makubwa. 

Mary Mganga wa Kata ya Busoka alisema pamoja na serikali kuweka ruzuku kwenye pembejeo za kilimo, hawana elimu ya matumizi yake na kuwa miongoni mwa sababu za kukosa mavuno ya kutosha. 

Kwa mujibu wa Mary, wakulima hao hawafahamu muda gani wanatakiwa kuweka mbolea ya kukuzia, kuondoa magugu shambani na dawa ya kuua wadudu. 

Alisema kukosekana kwa elimu hiyo kwao ni janga kwa kudidimia kiuchumi kwa kuvuna magunia 15 ya mpunga kwa hekari badala ya 40 mpaka 50. 

“Pia jembe la mkono sokoni linauzwa Sh.7,000 mpaka 10,000 ambao linatumika kulima eneo dogo, jembe linalokokotwa na ng’ombe linauzwa kwa Sh.200,000 gharama ambayo ni kubwa kulingana na hali zetu,” alisema Mary.

 Katika kuwasaidia wakulima wa hali duni wilayani hapa, Shirika lisilo la kiserikali la Dorfra Co.ltd kwa kushirikiana na Shirika la Meda wameanza kusambaza zana za kilimo kwa robo gharama na kutoa mafunzo kwa wakulima ili kupandisha thamani ya zao la mpunga na kuinua uchumi wa wakulima wanawake. 

Meneja wa Dorfra Co.ltd, Bakari Juma alisema kati ya Novemba 27 na 29 mwaka jana walitoa zana hizo kwa wakulima 525 wa kata 20 za Manispaa ya Kahama na kuwapatia elimu ya kilimo cha kisasa.

 Alisema elimu hiyo ni namna ya kulima kisasa, kanuni bora za kilimo, mbegu bora, utayarishaji wa shamba, matumizi sahihi ya mbolea, udhibiti wa magugu kwa kutumia dawa, magonjwa sumbufu na kupanda kwa kuzingatia mstari.

 Alisema wanawapatia wakulima hao majembe ya kukotwa  na  ng’ombe kila mmoja kwa gharama ya Sh.50,000 badala ya bei ya sokoni  Sh.200,000 ili kuhakikisha wanaongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

Mkuu wa Divisheni ya Kilimo na Uvuvi wa Manispaa hiyo, Pendo Matulanya, aliwataka wakulima hao kuwatumia maofisa ugani wa kata zao ili kupata ushauri wa namna ya kutunza shamba, kulima kisasa na muda gani wa kuweka mbolea ili kupata mavuno ya kutosha.