CHAMA Kikuu cha Ushirika cha Wakulima Mkoa wa Mara (WAMACU) kimewataka viongozi wa vyama vya ushirika kuelekeza nguvu zao kuwasaidia wakulima kuinuka kiuchumi.
Rai hiyo ilitolewa juzi na Meneja Mkuu wa WAMACU, Samwel Gisiboye wakati akizungumza na viongozi na wakufunzi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) waliopo mkoani Mara kwa ziara ya mafunzo kwa vitendo na kutoa ushauri wa kutunza amani na usalama kwa manufaa ya wananchi na Taifa.
Giseboye, alisema wakulima wanahitaji kuwezeshwa katika sekta mbalimbali na kuelimishwa ili kuleta mabadiliko kwa kuendesha kilimo cha kibiashara na kukuza uchumi.
Aliupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuwa wa kwanza kuwatembelea na kuwataka kuona namna ya kuongeza fani ya kilimo katika chuo chao ili kupanua wigo wa ajira kwa wahitimu wao nchini.
Aliwasihi katika maeneo yote wanakofanya ziara kunadi ajenda ya kilimo ili kuleta tija kwa taifa, kuongeza uzalishaji wa mazao na kuzalisha ajira.
Mkuu wa Msafara huo, Brigedia Jenerali Baganchwera Rutambuka, alikitaka chama hicho kujikita katika dhima waliyonayo ya kuwasaidia wakulima ili kuwainua kiuchumi kupitia mazao ya biashara.
Rutambuka, alikitaka chama hicho kuendelea kujikita kuwasaidia na kuwainua wakulima kwani kwa kufanya hivyo, watakuwa wamelikomboa Taifa kupitia Sekta ya Kilimo.
"Lengo letu ni kupita kuangalia amani na usalama wa jamii na mikakati ya Taifa hususani usalama wa mipaka kwa hali hiyo WAMACU jikite kwenye kilimo na si vingine,” alisema.
Mwenyekiti WAMACU, Momanyi Range aliwapongeza viongozi hao kwa kuwatembelea na kuwapa ushauri wa kuzingatia matakwa ya kiserikali na kuhakikisha wainua wakulima.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED