Ligi Kuu kurejea mapema

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:18 AM Jan 16 2025
Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda.
Picha: Mtandao
Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda.

BAADA ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kuahirisha fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), Bodi ya Ligi, imesema Ligi Kuu Tanzania Bara itarejea mapema.

Awali kufuatia michuano ya CHAN na Kombe la Mapinduzi, bodi hiyo ilitangaza Ligi Kuu Tanzania Bara itasimama hadi Machi Mosi, mwaka huu.

Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda, aliliambia gazeti hili sababu zilizopelekea kusogezwa kwa ligi hiyo sasa zote hazipo, hivyo kuna nafasi kubwa ya kurejea mapema baada ya viongozi wanaohusika na usimamizi na uendeshaji wa ligi kukutana.

"Tulitoa taarifa tunafanya hivyo kwa ajili ya kupisha mashindano mawili, Kombe la Mapinduzi na CHAN, moja limeisha lingine limesogezwa mbele na taarifa tumeipata kupitia tovuti yao, bado hatujapokea barua rasmi.

Hatuna sababu tena ya kuendelea kusubiri mpaka siku hizo. Niseme tu taarifa rasmi tutaitoa baada ya idara zote zinazohusika na usimamizi na uendeshaji wa ligi ofisini kukutana, tukimaliza tutatoa taarifa ya kurejea kwa ligi," alisema Ofisa Habari huyo.

Aliongeza kwao hakutakuwa na athari yoyote, na uamuzi huo umewarahisishia kumaliza ligi kwa wakati kwa sababu walikuwa 'wanaumiza kichwa' kuhusiana na muda ambao upo kikanuni.

"Hakutakuwa na kitu hasi, au kutupa tabu sana kwa sababu hata sisi tulikuwa tunaumiza kichwa kama tunaweza kumaliza ligi kwa wakati kutokana na ufinyu wa muda, " Boimanda alisema.