Wananchi Ngorongoro, Simanjiro wanufaika na huduma za mawasiliano ya Yas

By Cynthia Mwilolezi , Nipashe
Published at 03:16 PM Jan 16 2025
Wananchi Ngorongoro, Simanjiro wanufaika na huduma za mawasiliano ya Yas.
Picha: Mpigapicha Wetu
Wananchi Ngorongoro, Simanjiro wanufaika na huduma za mawasiliano ya Yas.

Wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, Simanjiro na Manyara wamenufaika na huduma za mawasiliano ya kasi ya 4G na 5G inayotolewa na Kampuni ya Mawasiliano ya Yas. Hatua hiyo imelenga kuwawezesha wananchi wa maeneo ya pembezoni kufikiwa na huduma za mawasiliano bora, hivyo kuwasaidia kujiinua kiuchumi.

Akizungumza leo jijini Arusha, Ofisa Mkuu wa Biashara wa Yas, Isack Nchunda, amesema kampuni hiyo imejikita kuboresha mawasiliano katika maeneo yenye changamoto. Ameeleza kuwa huduma hizi zimepelekwa katika Wilaya za Loliondo na Simanjiro, ambapo sasa wananchi wanapata fursa ya kutumia huduma bora za mawasiliano, utumaji na upokeaji wa fedha kupitia mtandao wa Yas.

"Huduma zetu za Tigo Pesa sasa zinajulikana kama Mixx by Yas, na tunaendelea na kampeni yetu ya 'Magift ya Kigift', ambayo inawapa wateja nafasi ya kushinda zawadi mbalimbali, ikiwemo fedha taslimu na gari. Tumefanya jitihada kubwa kufikia maeneo ambayo awali yalikuwa na changamoto za mawasiliano," amesema Nchunda.

Amebainisha kuwa mshindi wa kwanza wa gari aina ya Kia Seltos, Ibrahim Idd, anatoka Kanda ya Kaskazini na atakabidhiwa zawadi yake wiki ijayo mkoani Manyara. Kampeni hiyo pia imerahisisha mawasiliano kwa watalii, ambao sasa wanaweza kufaidika na huduma za kasi ya juu ya intaneti kwa shughuli zao za kimtandao.

1

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Kaskazini, Daniel Mainoya, amesema kampeni ya 'Magift ya Kigift' inaendelea, na washiriki wanapata zawadi za kila siku na kila wiki. Amefafanua kuwa zawadi zilizobaki ni pamoja na zaidi ya Shilingi milioni 156 na simu janja 172, huku akiwahimiza wateja waendelee kushiriki ili kunufaika.

Huduma mpya zinazotolewa na Yas ni sehemu ya mabadiliko ya chapa yaliyofanywa na kampuni hiyo, ambayo ilibadilisha jina kutoka Tigo kuwa Yas mnamo Novemba 26, 2024. Maboresho haya yanalenga kuboresha maisha ya wananchi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa maeneo ya pembezoni mwa nchi.

2