Mwanasiasa mkongwe na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja, amewatakia heri wana-CCM katika mkutano mkuu wa kushika mikoba ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Abdulahman Kinana.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mgeja amesema shauku kubwa ya wana-CCM ni kumpata Makamu Mwenyekiti atakayemsaidia mwenyekiti wa chama ambaye ni Rais Samia Suluhu Hassan.
"Nina imani kuwa atapatikana Makamu Mwenyekiti atakayemsaidia mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Samia kwani CCM ina hazina kubwa ya viongozi na wenye uwezo wa kuongoza katika nyanja mbalimbali," amesema Mgeja.
Mgeja amesema kuwa shauku kubwa ya Watanzania ni kuona nafasi ya Makamu Mwenyekiti ambaye atarithi mikoba ya Kinana na kuweza kutimiza majukumu yake mapya kwa ushirikiano wa wana-CCM na pia kumsaidia na kumshauri mwenyekiti wa CCM.
"Tunaamini kuwa atakayepatikana atakuwa ni mwenye kumshauri mwenyekiti wa CCM Rais Samia katika kuleta mabadiliko ndani ya chama hivyo ni vyema sasa tukasubiri Mkutano Mkuu wa CCM unatarajiwa kufanyika Januari 18 hadi 19, 2025, jijini Dodoma" amesema Mgeja.
Awali Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi wa CCM, CPA Amos Makalla alisema mkutano huo wa CCM utaambatana na vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, ambapo ajenda zitahusu kufanya uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, kupokea taarifa ya utekelezaji wa kazi za chama kwa kipindi cha mwaka 2022 hadi 2025, pamoja na taarifa ya utekelezaji wa Ilani kwa pande zote mbili, Bara na Zanzibar.
Kuhusu mchakato wa kumrithi Kinana, alisema mrithi wa nafasi hiyo anatarajiwa kupatikana baada ya Kamati Kuu kuwasilisha mapendekezo ya jina kwa halmashauri kuu kisha halmashauri kuu kuwasilisha jina hilo kwa wajumbe wa mkutano mkuu kwa ajili ya kupigiwa kura.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED