WALIMU wa masomo ya Sayansi katika Mkoa wa Mwanza, wamepewa jukumu la kuifanya jamii kuwa ya kisayansi kwa kuhakikisha kila mtu anayepita shuleni anapata maarifa yanayoongeza thamani ya maisha yake, akielewa na kutumia sayansi katika nyanja mbalimbali za maisha.
Hayo yamesemwa Januari 16, 2024 na Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Martin Mkwabi, wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa walimu wa sekondari wanaofundisha masomo ya Sayansi, Hisabati, na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), yanayofanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nganza, mkoani humo.
Mkwabi amesema ili kufanikisha lengo hilo, ni lazima kuwa na walimu wenye uwezo wa kufundisha na kuwavutia wanafunzi wengi kupenda masomo ya sayansi, ambao baadaye watakuwa wataalamu wa kushughulikia masuala mbalimbali kwenye jamii.
Ameongeza kuwa, licha ya changamoto za rasilimali, mwalimu mwenye ufanisi atajua jinsi ya kuchagua mbinu sahihi za ufundishaji na kutumia zana zilizopo katika eneo lake ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.
Akitolea mfano kuwa hata kama vitabu vichache au vifaa vya maabara vipo, mwalimu mwenye ujuzi anaweza kutumia rasilimali kidogo zilizopo kufundisha darasa kubwa kwa ufanisi na wanafunzi wakaelewa.
“Walimu wenye uwezo wa kufundisha na kuwavutia wanafunzi wengi kusoma masomo ya sayansi watatengeneza jamii ya kisayansi, inayojua kujikinga na maradhi, kutumia rasilimali zilizopo kwa usahihi, kuzingatia mahitaji ya sasa, kuwa raia wa dunia,a,baye ataishi kwa namna yeyote kwa kutumia sayansi,” amesema Mkwabi.
Mkwabi amesisitiza pia kuwa heshima ya Mtumishi wa Umma inatokana na huduma anayotoa kwa jamii, na kwamba ulimwengu wa sasa unahitaji maarifa zaidi ya vyeti pekee, aliongeza kuwa, mafunzo hayo yanatarajiwa kuleta tija kubwa kwa maendeleo ya elimu nchini.
“Nimefurahi kwamba miongoni mwa ajenda zitazofundishwa na wawezeshaji wetu ni suala la Sera ya Elimu ya mwaka 2014, toleo la 2023, na mitaala iliyoboreshwa, mtafundishwa vyema utekelezaji wake na faida zake ili nanyi mkaielimishe jamii kuhusu sera hii inayozingatia mabadiliko ya dunia kwa sasa,” ameeleza Mkwabi.
Mratibu wa Mafunzo ya Kituo cha Mwanza kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Majaliwa Mkalawa, ameeleza kuwa Wizara, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP), inaendelea kutoa mafunzo kwa walimu wa masomo ya Fizikia, Kemia, Biolojia na Hisabati pamoja na wathibiti ubora wa masomo hayo.
Amesema dhima kuu ya mafunzo hayo ni kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari nchini kwa kuwajengea uwezo walimu, ili waweze kutumia mbinu shirikishi na kumudu mahitaji mbalimbali ya ufundishaji.
Amefafanua kuwa mafunzo hayo pia yanazingatia matumizi ya mbinu za kisasa katika ufundishaji na ujifunzaji ili kuendana na wakati, huku wakizingatia matumizi ya zana za ufundishaji zinazopatikana kulingana na mazingira wanayoyazunguka.
“Mafunzo haya yataangazia umahiri katika ufundishaji na kusaidia walimu kuwa na uwezo wa kuandaa masomo yao kwa ufanisi ili yaweze kueleweka kwa wanafunzi. Vilevile, walimu watapata ujuzi wa kutumia Lugha ya kiingereza, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika ufundishaji na kujifunzia,” amesema Majaliwa.
Amesisitiza kuwa walimu wanatakiwa kuwa mabalozi wa kuhamasisha wanafunzi, hususan wasichana, kupenda masomo ya sayansi, na kwamba anaamini baada ya mafunzo, ufaulu katika masomo hayo utaongezeka.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED