Rais Samia kuzindua Mkutano Mkuu wa ALAT Mwanza

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 04:21 PM Jan 17 2025
news
Picha: Mtandao
Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), utakaofanyika Februari mwaka huu jijini Mwanza.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Murshid Ngeze, wakati akifungua kikao cha Kamati Tendaji jana jijini Dodoma. Kikao hicho kililenga kujadili ajenda mbalimbali, ikiwemo maandalizi ya Mkutano Mkuu wa mwaka wa jumuiya hiyo.

Ngeze amesema mkutano huo, ambao ni wa mwisho chini ya uongozi wa sasa wa ALAT, umepangwa kufanyika jijini Mwanza mwezi ujao, huku Rais Samia Suluhu Hassan, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.

“Ningependa kugusia kuhusu mkutano wetu wa mwisho katika uongozi huu. Tumemwalika Mheshimiwa Rais kuwa mgeni rasmi, na hapa namuagiza Katibu kuhakikisha maandalizi yote yanakamilika kwa wakati, ili tumwandikie barua ya kumkumbusha Rais kuhusu mwaliko wetu,” amesema Ngeze.

Aidha, Ngeze amesisitiza umuhimu wa mshikamano ndani ya jumuiya hiyo kama nguzo kuu ya mafanikio. “Napenda kuwapongeza kwa mshikamano uliopo miongoni mwetu. Naomba mshikamano huu uendelee, kwani taasisi yoyote haiwezi kufanikiwa bila umoja. Nawashukuru sana kwa hali ilivyo sasa,” ameongeza.

Kuhusu kuimarisha mahusiano ya ndani na nje ya jumuiya hiyo, Ngeze amesema Katibu anapaswa kuandaa barua za maombi ya ziara katika nchi mbili, ambapo Kamati Tendaji inaweza kugawanyika ili kufanya ziara hizo kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

Mkutano huo unatarajiwa kuleta viongozi wa ngazi mbalimbali kutoka maeneo yote nchini, huku ukilenga kuimarisha utendaji wa serikali za mitaa na ushirikiano kati ya viongozi wa jumuiya hiyo.