Wafanyabiashara mkoani Shinyanga wameeleza changamoto zinazowakabili kutokana na utitiri wa kodi, ikiwemo kodi moja kutozwa na taasisi mbili tofauti, na kuomba kodi ya ushuru wa huduma (Service Levy) iondolewe kwa kuwa inatozwa kwenye mtaji badala ya faida.
Wakizungumza Januari 17, 2025, kwenye mkutano wa Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, walitoa mapendekezo ya kuboresha mifumo ya ulipaji kodi. Mfanyabiashara Mayengo Bageni kutoka Kahama amelalamikia kodi ya Service Levy, akisema inawadidimiza kiuchumi. Alipendekeza iondolewe na taasisi moja pekee ipewe jukumu la kutoza kodi ili kuondoa ukiritimba.
Gilitu Makula amekazia hoja ya kuondoa Service Levy kwa sababu haiendani na hali halisi ya kibiashara, huku Katibu wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini (SHIREMA), Gregory Kibusi, akiomba kupunguzwa kwa mlolongo wa kodi kwa wachimbaji ili kupunguza utoroshaji wa madini.
Mwakilishi wa wakulima, Kulwa Dotto, amependekeza kuondolewa tozo kwenye mazao yanayotolewa mashambani kwenda nyumbani kwa kuhifadhi badala ya biashara.
Kaimu Mratibu wa TUCTA Mkoa wa Shinyanga, Laurean Kyombo, ameshauri kuondoa kodi kwenye posho za wafanyakazi wa sekta binafsi, zawadi za Mei Mosi, na mafao ya wastaafu.
Mapendekezo mengine ni pamoja na kurudisha viparata kwa wajasiriamali, kuondoa kodi kwenye vifaa vya watu wenye ulemavu, na kupunguza tozo kwenye mitambo ya madini.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, ameipongeza tume hiyo kwa kusikiliza changamoto za walipa kodi na kusisitiza umuhimu wa kodi kwa maendeleo ya taifa. Alisema, "Tafiti zinaonyesha miaka 50 ijayo Tanzania inaweza kuwa miongoni mwa nchi nne zenye uchumi mkubwa barani Afrika endapo kodi zitalipwa ipasavyo."
Kaimu Mwenyekiti wa Tume ya Maboresho ya Kodi, Leonard Mususa, amesema Rais Samia aliunda tume hiyo Oktoba 4, 2024, kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu kodi nyingi na mazingira magumu ya ulipaji kodi. Tume hiyo inalenga kuboresha mifumo ya kodi ili kuongeza mapato na kuvutia uwekezaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED