KATIKA kuhamasisha umma kutii sheria bila shuruti, polisi mkoani Mbeya kwa kushirikiana na taasisi zinazosimamia hakijinai za magereza na mahakama walianzisha kampeni.
Ililenga kuelimisha jamii kutambua umuhimu wa dhima hiyo ya kutii sheria bila kulazimishwa.
Elimu hiyo iligusa makundi mbalimbali wakiwamo madereva ili wanapoendesha vyombo vya moto wazingatie sheria za usalama barabarani badala ya kusubiri walazimishwe au washurutishwe.
Hata hivyo, pamoja na kampeni hiyo, bado utii wa sheria bila shuruti umekuwa ni changamoto mkoani humo na baadhi ya madereva huvunja sheria na kuendelea kusababisha makusanyo makubwa ya faini.
Wingi huo wa makusanyo yanayotokana na makosa mbalimbali ya barabarani, unajidhihirisha katika taarifa ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya Benjamin Kuzaga anayoitoa hivi karibuni.
Kamanda Kuzaga anasema jeshi hilo limekusanya zaidi ya Sh. bilioni 3.4 kutokana na makosa mbalimbali ya ukiukwaji sheria za usalama barabarani katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2024.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la Sh. milioni 104.8 kulinganisha na mapato ya mwaka 2023 zilikokusanywa bilioni 3.3.
Niwapongeze polisi kwa mafanikio hayo, lakini nikija na ushauri kwamba, elimu kwa madereva inapaswa kupewa kipaumbele zaidi kuliko faini zinazotozwa kila uchao.
Uwapo wa makusanyo mengi ya fedha zinazotokana na faini za makosa mbalimbali, ni wazi kwamba kuna sehemu hapako sawa, hivyo ipo haja kwa jeshi hilo kujikita zaidi kwenye utoaji wa elimu kwa madereva.
Ninaeleza hivyo, kwa sababu kila kukicha madereva wapya wanaingia barabarani ambao nao ni vyema wakapata elimu ya jinsi ya kutii sheria za usalama barabarani bila shuruti.
Ingawa inawezekana wapo baadhi ya madereva wasiotii sheria kwa makusudi, lakini njia hiyo inaweza kusaidia kupunguza wingi wa makusanyo hayo, yanayotangazwa.
Wingi huo wa makusanyo ni dalili kwamba kuna sehemu hakujawa na mafanikio. Kupitia kampeni ya elimu ya kutii sheria bila shuruti, binafsi nilitarajia kupungua kwa faini kwani madereva wangetii sheria bila kulazimishwa.
Sio kwamba ninapinga kazi inayofanywa na jeshi hilo, ila ninalenga kujikita zaidi katika utoaji wa elimu ya usalama barabarani, kwani kila kukicha madereva wapya wanaingia barabarani.
Hivyo, elimu ikiendelea kutolewa kila wakati ili madereva wengi wawe wa zamani na wapya wataipate, wale ambao wataendelea kukaidi, watozwe faini zaidi, japo ni imani yangu kuwa elimu inaweza kupunguza faini.
Elimu hiyo inaweza kusaidia kutimiza moja ya malengo ya kampeni ya kutii sheria bila shuruti ambayo ni kuboresha maadili ya jamii kama msingi wa maendeleo yanayozingatia usalama, amani na utulivu ambavyo ni nguzo za ustawi wa kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.
Ikumbukwe kuwa msingi wa kampeni hiyo ulikuwa ni kuongeza ari na moyo wa uzalendo unaozingatia uwajibikaji katika harakati za kujiletea maendeleo bila kuvunja sheria za nchi.
Ninaamini madereva wakipewa elimu ya matumizi sahihi ya barabarani, itasaidia kupunguza ajali au makosa ambayo yanachangia kuwapo kwa ajali zinazokatisha maisha ya watu au kuwa na ulemavu wa kudumu.
Hivyo, njia bora ya kuwafanya madereva wawe na uelewa wa kutosha wa matumizi sahihi ya barabara, si kujikita kwenye makusanyo ya faini bali ingekuwa ni kuangalia chanzo cha makosa na kukifanyia kazi.
Kimsingi elimu ni ya muhimu kwa maisha, katika shughuli za kila siku, awe mwanamke au mwanamume inampasa kupata elimu ili imsaidie kufanya maamuzi sahihi na kwa usahihi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED