Nishati safi mkombozi wa mazingira

Nipashe
Published at 08:14 AM Jan 14 2025
Nishati safi.
Picha:Mtandao
Nishati safi.

MIAKA ya nyuma kabla ya kampeni ya matumizi ya nishati safi haijapamba moto, usafirishaji mkaa kutoka mikoani ulishamiri na uharibifu wa mazingira ulikuwa katika hali mbaya.

Kwa mifano michache kwa wanaopita Barabara ya Bagamoyo, ilikuwa huwezi kutembea bila kukutana na pikipiki au malori yaliyosheheni magunia ya mkaa.

Ukiangalia idadi ya magunia yaliyopakiwa kwenye malori hayo, utagundua ni jinsi gani misitu ilivyokuwa ikiangamia kwa kukatwa miti inayochomwa na kuwa mkaa.

Mbali na uharibifu wa mazingira, lakini matumizi ya kuni na mkaa yana athari kubwa katika afya za binadamu kutokana na moshi wanaouvuta.

Matumizi ya nishati safi ya gesi imesaidia kwa kiasi kikubwa kuepuka uchafuzi wa hewa ambao unasababisha uharibifu wa mazingira na pia kusababisha magonjwa mbalimbali.

Ulinzi wa afya ya mama, familia, mazingira na taifa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ni lazima uanzie jikoni.

Mkutano Mkuu wa Maboresho ya Serikali za Mitaa (TOA), ulieleza kuhusu tamanio la serikali kufikia asilimia 80 ya Watanzania wote kutumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.

Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa kinara wa kutangaza matumizi ya nishati safi ya kupikia na lazima taifa lianze sasa kubadilisha nishati inayotumiwa kupikia.

Mara kwa mara anapokuwa kwenye majukwaa mbalimbali ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, Rais anasema huwezi kumaliza au kupunguza ukataji miti unaoangamiza misitu kama hutaligusa jiko. 

Kampeni ya Rais imefanya mengi, Watanzania wameelezwa umuhimu wa matumizi ya teknolojia za kupikia zinazopunguza madhara kiafya, athari kwa mazingira na kijamii.

Na sasa Rais amelifikisha taifa kwenye kutekeleza Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia 2024 – 2034.

Analenga kaya zenye ‘jiko safi na salama’, ambayo asilimia 80 ya Watanzania watakuwa wanatumia jiko lenye nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.

Pamoja na kuwaondoa kinamama katika matumizi ya kuni na mkaa na kutumia nishati safi, pia taasisi kubwa ambazo zinahudumia watu wengi kupata chakula, zinahimizwa kuhama kwenye matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia kwenye nishati safi ili kupunguza uharibifu wa hewa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo, ili kufanikiwa katika matumizi ya nishati safi ipo haja ya kuwa uhamasishaji wa kutumia majiko yanayotumia nishati safi na yapatikane kwa urahisi ili wanayoyahitaji wasipate vikwazo kwa kuyapata.

Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) inaeleza kuwa Tanzania Bara ina takribani kaya milioni 13.9. 

Kufikia azma hiyo kaya zenye jiko safi na wakuu wa mikoa na wilaya wasimamie matumizi ya nishati safi ya kupikia na pia wizara na taasisi za umma kadhalika na sekta binafsi kuzingatia matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira na kuepusha athari nyingi zinazotokana na kutumia nishati zisizo safi.

Mwaka jana Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira iliagiza taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 100, ifikapo Januari, mwaka huu, ziache kutumia kuni na mkaa kupikia.

Ofisi ya Makamu wa Rais, katika mikakati yake inaeleza kuwa hilo limefanyika na taasisi nyingi zikiwamo za umma kuanzia Magereza, kambi za jeshi, shule za sekondari, vyuo vya ualimu na vikuu vimeanza kutumia nishati safi ya kupikia.

Pia, juhudi zinafanywa na kila taasisi inayohusika na nishati na katika mbio za Mwenge wa Uhuru, mwaka huu, ujumbe mkubwa unaobebwa ni uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi kupikia.

Uhamasishaji huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na kuepusha athari zinazosababishwa na hewa chafu inayotokana na kuvuta moshi mchafu.