WATU wanaojitambua, ni wazi hujiwekea malengo na muda maalum wa kuyatimiza, hutumia mwisho wa mwaka kutathmini na mwanzo wa mwaka (mwaka mpya), kuanza utekelezaji, kulingana na mikakati waliojiwekea.
Mipango ipo katika ngazi mbalimbali kuanzia kwenye familia, vikundi mbalimbali vya kijamii, taasisi binafsi na za serikali na taifa kwa ujumla wake.
Huwa na mipango ambayo hutekelezwa kulingana na malengo husika na matokeo yake, hutarajiwa baada ya muda waliojiwekea.
Katika mipango, ipo ambayo utekelezaji wake na matokeo yake huonekana ndani ya muda mfupi, lakini pia ipo mipango ya muda mrefu ambayo utekelezaji wake unaweza kupangwa kutekelezwa kwa awamu awamu.
Mwaka 2025 ni mpya. Mbali na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hiyo ya kuendelea kuishi, ni wazi kwamba kila mmoja wetu anawajibika kutathimini aliyoyafanya mwaka 2024.
Hapo kuna maswali, je yalikuwa na maendeleo katika ngazi gani, kulingana na nafasi yake aliyonayo kuanzia kwenye ngazi ya kifamilia hadi kwenye uongozi wa taasisi, iwe ya binafsi au taasisi.
Kuanzia mtoto mwenye umri ambao anaweza kuelewa maana ya elimu anapaswa kujitathimini kiwango chake cha ufaulu wa mwaka jana, akilinganisha na mwaka uliopita.
Pia, akaweka dhamira yake ya kutimiza malengo kwenye masomo kwa mwaka huu mpya 2025.
Maisha ni mapambano! Kama kuna mipango ya maendeleo uliipanga au yalipangwa na taasisi, kisha haikufanikiwa, kutokana na changamoto za aina mbalimbali, ni jambp jema kujipanga upya, ikiwamo kubadili mbinu badala ya kukata tamaa.
Kukata tamaa, ni kupishana na mafanikio, kwa kushindwa kuongeza bidii kwa kiwango kidogo.
Katika andiko la Mapendekezo ya Mpango wa Watu Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022-2025/2026, pamoja na mambo mengine kadhaa, limeeleza juhudi kadhaa ambazo zimefanywa kutelekeleza mpango huo.
Juhudi hizo ni pamoja na: kuendelea kutoa elimu bila ada; kuendelea kuboresha upatikanaji wa maji mijini na vijijini; kuendelea kuboresha ushiriki wa sekta binafsi katika kutoa huduma za afya hususan maeneo ya vijijini.
Mengine ni suala la kuendelea na ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali; na kuendelea na ujenzi wa barabara za kufungua fursa za kiuchumi katika maeneo ya mijini na vijijini.
Kutokana na utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali za maendeleo, kumekuwapo matokeo chanya katika viashiria vya maendeleo ya watu.
Hapo inakuwamo kuongezeka wastani wa umri wa kuishi kutoka miaka 66.1 mwaka 2019 hadi miaka 68.3 (2023/2024) na makadirio ya kufikia miaka 68.0 kwa mwaka 2025.
Aidha, wastani wa umri wa kuishi kwa kuzingatia jinsia, unakadiriwa kufikia miaka 70.4 kwa wanawake na miaka 65.5 kwa wanaume mwaka 2024. Huu mfano wa mipango ya mafanikio kwa ngazi ya taifa.
Hivyo, haya katika ngazi familia zinapaswa kuangalia ni wapi zilifanikiwa na kama zilikwama, ilikuwaje zikajikuta kwenye hali ya mkwamo.
Pia, hata viongozi wa taasisi binafsi na zile za serikali nao waangalie ni utekelezaji wa mipango kwenye maeneo yao ya kazi.
Daima usione aibu, kubadili marafiki hasa kama umebaini kuwa wana tabia ambazo zimegharimu mafanikio ya mipango yako kukwama, au hawana ushawishi wa kufanya mambo ya maendeleo zaidi wanaendekeza anasa.
Chukua nafasi ya kutafakari sasa, kwamba je mafanikio yako yanachochewa na mambo gani? Kama kuna kikundi au mtu aliyefanikiwa, usisite kuiga, maana wahenga wanasema kizuri huigwa.
Hivyo, siyo mbaya kuiga mbinu za kuhakikisha unafanikisha mipango yako iliyo ya halali.
· Mwandishi anapatikana kwa anwani: [email protected];
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED