MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania TCRA imeendelea na kampeni yake ya ‘Ni Rahisi Sana’ msimu wa pili katika viwanja vya Nyamanzi Fumba Zanzibar.
Kampeni hiyo inafanyika katika maonesho ya kimataifa ya biashara kuelekea maadhimisho ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yaliyofunguliwa rasmi na Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo, Januari 5, mwaka huu.
Msimu huu wa pili ulioanza rasmi Januari Mosi, mwaka huu, kampeni hiyo imejikita katika kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kikoa cha DOT TZ.
Maofisa walioko katika banda la TCRA, Sophia Mabada na Jasmine Kiyungi, walisema kutumia kikoa cha DOT TZ kutasaidia kumtambulisha mhusika au mfanyabiashara kama ni mzawa au mwenyeji wa Tanzania au biashara hiyo makao makuu yake yapo Tanzania moja kwa moja bila kutafuta taarifa nyingine.
“Suala hili litamwezesha mhusika kukubalika na kuaminiwa kwa urahisi, hivyo kufanikisha kufanya shughuli zake mbalimbali kwa urahisi,” alisema Mabada.
Kiyungi alisema kikoa cha DOT TZ kina umuhimu mkubwa kwa kuwa kinamhakikishia mtumiaji wa kikoa hicho ulinzi na usalama kwa kuwa kimesajiliwa Tanzania, hivyo taarifa na miundombinu yote ya kikoa hicho bado vitakuwa viko Tanzania.
“Kwa hiyo hata kama kuna hitilafu yeyote kwa kuwa miundomninu yote ya kikoa cha DOT TZ iko Tanzania basi itakuwa ni rahisi kutatua, hivyo turudi nyumbani kwenye kikoa chetu,” alisema.
Kampeni ya ‘Ni Rahisi Sana’ tangu kuanza Oktoba Mosi, 2024, imeleta matokeo makubwa kwa vijana, watoto, wazee na wadau wa mawasiliano.
Takwimu zinaonesha kuwa kampeni hiyo imesaidia watu mbalimbali kuepuka kadhia zinazopatikana wakiwa katika matumizi mbalimbali ya huduma za mawasiliano ya simu na intaneti kama vile kutapeliwa mtandaoni na kwamba kumekuwa na mwitikio mkubwa wa kuripoti matukio ya uhalifu mtandaoni kupitia namba 15040.
Kampeni hiyo imesaidia kupunguza matumizi ya laini za simu zilizokuwa zimesajiliwa bila matumizi halali kutokana na hamasa ya kuhakiki namba zilizosajiliwa na kitambulisho cha NIDA kupitia namba *106#.
Kwa kuhakiki huko kulisababisha watu waliogundua kuwa vitambulisho vyao vimesajili laini za simu wasizozitumia kwa matumizi halali waliweza kuwasiliana na watoa huduma wao na kuomba kufutwa kwa namba hizo.
Meneja wa TCRA Ofisi ya Zanzibar, Esuvatie Masinga, alisema pamoja na kuendelea na msimu huu wa pili wa kampeni ya ‘Ni Rahisi Sana’, bado hawataacha kuelimisha umma kuhusu fursa muhimu zinazopatikana katika huduma za mawasiliano.
Masinga alisisitiza kuwa jamii inapaswa ichangamkie fursa zinazopatikana kwenye huduma za mawasiliano kama vile ajira na biashara kwa kutangaza biashara hizo mitandaoni na hivyo kujipatia kipato na kukuza uchumi wao.
Alisema dunia kwa sasa imefika mabadiliko makubwa na kila kitu kwa sasa kinaendeshwa kidigitali, hivyo wataendelea kuelimisha watu hasa watoto wadogo na wabunifu mbalimbali kuanza kuitambua na kuipenda teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ili wanapokuwa wawe wameshapata uzoefu mkubwa na ujuzi mkubwa wa kuitumia teknolojia hiyo katika kuendesha shughuli za kiuchumi na kijamii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED