Bodaboda waandamana kisha kufunga barabara kisa kunyanyaswa na polisi

By Remmy Moka , Nipashe
Published at 08:13 AM Jan 11 2025
Bodaboda waandamana kisha kufunga barabara kisa kunyanyaswa na polisi.
Picha: Mtandao
Bodaboda waandamana kisha kufunga barabara kisa kunyanyaswa na polisi.

WAENDESHA pikipiki, maarufu ‘bodaboda’ pamoja na bajaji mkoani Kigoma wameandamana na kufunga barabara katika eneo la mzunguko kwa madai kwamba wamechoka kunyanyaswa na kukamatwa ovyo na Jeshi la Polisi mkoani humo.

Maandamano hayo yaliyofanyika juzi yaliingiliwa kati na kuzimwa na Jeshi la Polisi ambalo lilitumia silaha yakiwamo mabomu ya machozi huku baadhi ya madereva hao wakitiwa mbaroni kwa madai ya kusababisha vurugu hizo. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa maandamano hayo, bodaboda hao akiwamo Chita Jackson, walisema wamekuwa wakifanya shughuli hizo bila uhuru  licha ya wao kuwa sehemu ya upatikanaji wa pato la taifa. 

Jackson alidai kuwa manyanyaso hayo ni pamoja na kukamatwa mara kwa mara bila sababu maalum licha ya kujitahidi kufuata sheria na taratibu wanazoelekezwa kwa ajili ya usalama barabarani. 

Alisema kila wakikamatwa kwao wamekuwa wakitozwa faini hadi Sh. 100,000 ili kupata dhamana katika vituo vya polisi hali inayowafanya baadhi yao kushindwa kuendelea na kazi hiyo na kuingia katika hatihati ya kujiingiza katika makundi ya wezi. 

Bodaboda mwingine, Hamis Abdullah, aliwashtumu askari wa usalama barabarani kuwakamata kwa vurugu na wakati mwingine kuwasababishia ajali huku wakiwatoza faini za kuanzia Sh.50,000 hadi 150,000 pale wanapokutwa na makaso mbalimbali yakiwamo kutovaa kofia ngumu. 

Mwenyekiti wa Waendesha Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Kigoma, Samwel Mtema, alisema hajapendezwa na hatua hiyo iliyofikiwa na madereva wenzake na kuwa tayari walikuwa wameanza kuongea suala hilo na viongozi wa kamati ya usalama barabarani mkoa. 

Alisema madhumuni ya kamati ya usalama mkoa kuja na operesheni iliyopo kwa sasa ni ni kukagua vyombo ambavyo havijakidhi vigezo pamoja na madereva wasiofuata sheria na taratibu. 

Alisema operesheni hiyo inalenga kusaidia usalama wa waendesha bodaboda pamoja na watumiaji wengine wa barabara na vyombo hivyo hivyo kuwataka kutii sheria bila shuruti. 

Akizungumza katika eneo la tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Philemon Makungu, alisema baadhi ya bodaboda hawana leseni akitaja sababu kuu kuwa si raia wa Tanzania, hivyo hawana vitambulisho vya taifa (NIDA).   

Kamanda Makungu alisema wametoa elimu kwao mara kwa mara kuhakikisha wanafuata sheria za barabarani bila mafanikio hivyo kuanzisha operesheni hiyo inayowalenga wale tu wasiofuata sheria ikiwamo kuvaa kofia ngumu, kuwa na leseni, bima za pikipiki pamoja na kufuata sheria za usalama barabarani. 

Alisema wanazungumza na viongozi wao kwa kuwa malengo ya jeshi hilo ni kuhakikisha amani na utulivu katika Mkoa huo huku akiwataka wale wote wanao lituhumu jeshi hilo, ama maofisa wake kwa namna yoyote kuwasilisha tuhuma hizo pahala husika ili zipatiwe suluhu. 

“Tuhuma ni tuhuma tu walete tuhuma zao zisikilizwe na kupatiwa suluhu na si kufanya vurugu na kuongea bila kuwa na suluhu,’’ alisema Kamanda Makungu.